TAHARIRI: Kenya ijifunze kujitegemea, ipo hatari yaja ulimwenguni
KADRI mienendo ya kimataifa inavyozidi kubadilika, mataifa yanayostawi hasa barani Afrika yanazidi kusukumwa kwenye mahangaiko makubwa.
Utawala wa sasa wa Amerika chini ya Rais Donald Trump, unafaa utumike kuyazindua usingizini mataifa ya ulimwengu.
Sera za Trump ambazo zimeushtua ulimwengu ni kandamizi zaidi hasa kwa nchi za Afrika.
Trump, akijaribu kutekeleza falsafa yake ya America First (Amerika Kwanza), amekomesha au kufuta misaada ya kigeni, amekatiza mikataba ya kimataifa, ameyawekea mataifa mengi vikwazo vya kiuchumi na kulazimisha nchi yake ikubaliwe kunufaika kwa madini ya mataifa ya kigeni.
Kwa kukomesha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, kwa mfano, ameashiria kuwa Urusi inaweza kuvamia nchi hiyo jirani ya Ulaya na kuangamiza wananchi wasiokuwa na hatia.
Ni ishara kuwa mataifa yanayostawi ambayo yamezoea kutegemea usaidizi wa mataifa yanayoendelea yapo tu kutokana na huruma ya wahisani wake. Wahisani hao wakiamua kujiondoa, wategemezi watajipata hatarini.
Inashangaza kuwa ulimwengu unapojitahidi kujiendeleza kiteknolojia, kijeshi, kisayansi na fani nyinginezo, hakuna taifa la Afrika linalowazia kuanza kutengeneza bidhaa za kimsingi kama vile simu za mkononi, baiskeli, pikipiki, magari au hata kujiundia silaha.
Hata sufuria, nyembe, vichokonoo tunaagiza kutoka China!
Ni muhimu Afrika ianze safari ya kujiweka huru katika teknolojia, uchumi, na ulinzi.
Je, kwa nini hatujawahi kufikiria kuunda hata bunduki? Ikumbukwe kuwa mataifa yaliyoendelea kwa sasa yanatengeneza silaha za kinyuklia, makombora ya mbali na hata droni.
Itakuwaje iwapo afriti mmoja mwenye mamlaka ataamka siku moja na hasira zake kisha aamue kuungamiza ulimwengu?
Au tutafanya nini iwapo ‘jambazi’ mmoja mwenye mamlaka atakapoamua kuyavamia mataifa yetu kwa ajili ya kuchimba madini yetu yenye thamani kubwa? Kinachosikitisha hata zaidi ni kuwa hata madini yenyewe hatuna teknolojia ya kuyachimbua kutoka ardhini. Hata mafuta yetu hatuwezi kuyachimba!
Safari ya maelfu ya maili huanza na hatua ya kwanza, chambilecho wahenga. Polepole tunaweza kuanza kujinyanyua wenyewe kiteknolojia na kisayansi kwa minajili ya kujitegemea.
Mafanikio ya nchi kama China katika kujenga viwanda vyayo yenyewe na ustadi wayo wa kiteknolojia yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa mustakabali bora na salama wa Afrika.
Zaidi ya hayo, Afrika inapaswa kuanza kujitosheleza kwa mahitaji ya kimsingi.