Uhaba wa madaktari wa upasuaji Afrika watatiza wagonjwa
KATIKA kijiji cha Koono, Kaunti ya Turkana, Lomong, kijana wa miaka 12 amekaa kwenye kiti huku akiwatazama vijana wenzake wakicheza kandanda.
Anauguza mguu wake uliofanyiwa upasuaji juma lililopita kurekebisha tatizo lililosababishwa na jeraha alilopata alipokuwa akicheza.
“Ilikuwa Januari mwaka jana ambapo alikuwa akicheza na wenzake kwa bahati mbaya akaanguka na mguu wake wa kulia ukavunjika,” aeleza baba yake, Bw Ajak.
Kwa miezi kadhaa tokea wakati huo, Ajak, alikuwa akimbeba mwanawe kumpeleka katika kliniki moja iliyoko kilomita chache kutoka kijijini mwao, lakini hakuwa akipokea matibabu.
“Alikuwa akipokea tu huduma za kupunguza maumivu na kufungwa au kubadilishwa bendeji. Hii ni kwa sababu kliniki hiyo haina uwezo wa kuendesha shughuli za upasuaji.”
Kwa hivyo, wazazi wake Lomong walilazimika kusafiri kwenda mjini Lodwar mara kadhaa kufuatilia ombi la kutaka mtoto wao afanyiwe upasuaji katika hospitali yenye uwezo wa kufanya utaratibu huo.
“Umbali wa kijiji chetu hadi katika hospitali hiyo ni takriban kilomita 70, na gharama ya usafiri ni ya juu. Aidha, kila tulipokuwa tukienda huko, tulikuwa tukipata foleni ndefu,” aongeza Ajak.
Aidha, anaeleza kuwa pia hospitali hiyo ilikuwa ikikumbwa na tatizo la uhaba wa wahudumu wa kutosha, huku idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri kufanyiwa upasuaji pia ikiwa kubwa.
Ni suala lililowalazimu kusubiri kwa muda huu wote kabla ya mwanao kufanyiwa upasuaji huo ambapo kwa sasa Lomong anaendelea kupata nafuu.
Tatizo la uhaba wa madaktari wa upasuaji, vile vile hospitali na miundo misingi ya kufanyia taratibu hizi halikumbi tu Kaunti ya Turkana au Kenya, ni shida ya bara la Afrika.
Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya raia wa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara, hawawezi kufikia huduma hata sahili ya upasuaji.
Hii ndio ilikuwa mada kuu madaktari, watafiti na washikadau katika sekta ya matibabu ya upasuaji barani walipokutana mwezi Februari jijini Kigali, katika kongamano la kwanza la matibabu ya upasuaji barani (Pan-African Surgical Conference).
Kulingana na wataalam, hali ya huduma za upasuaji barani ni ya kutatanisha kwani mbali na kuwa ya kudunisha, haifadhiliwi vilivyo, huku mapengo yaliyopo katika miundo misingi yakiawazuia mamilioni ya watu wasiweze kufikia huduma hizi.
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha kwamba idadi ya madaktari wa upasujai barani ni sawa na madaktari 0.5 kwa kila idadi ya watu 100,000. Idadi hii ni ya chini zaidi ikilinganishwa na viwango vinavyokubalika vya madaktari wa upasuaji 38 kwa kila watu 100,000.
Kulingana na Prof. Abebe Bekele, Profesa wa upasujai na Naibu Chansela wa masuala ya akademia na utafiti katika Chuo Kikuu cha Global Health Equity, janga la ukosefu wa madaktari wa upasuaji barani linatokana na kutokuwepo kwa msingi wa kustawisha wataalam katika sekta hii.
“Katika mataifa mengi hapa barani hakuna mfumo unaohakikisha mafunzo ya wataalam hawa,” aongeza Prof Bekele.
Dkt Charles Kabetu, mtaalamu wa unusukaputi na afisa wa matibabu anayesimamia eneo la Afrika Mashariki, asema, upungufu huu hauathiri tu madaktari wa upasujai, bali pia wahudumu wote wanaohusika katika utaratibu huu.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, mataifa ya Afrika yanaendelea kukumbwa na uhaba wa wahudumu wa upasuaji huku baadhi ya nchi zingne zikiwa na wahudumu 2.3 kwa kila watu 1000.
“Uhaba huu unafanya hali kuwa mbaya zaidi, na hivyo, kuzuia hospitali zisitoe huduma jinsi ipaswavyo,” anaongeza Dkt Kabetu.
Hali ni mbaya hata zaidi katika maeneo ya mashambani huku madaktari na wahudumu wengi wa upasuaji wakifanya kazi mijini, suala ambalo limeacha hospitali za maeneo ya mashambani bila wataalam.
Hali ni mbaya hata zaidi katika maeneo ya mashambani huku madaktari na wahudumu wengi wa upasuaji wakifanya kazi mijini, suala ambalo limeacha hospitali za maeneo ya mashambani bila wataalam.
“Wengi hukimbilia hospitali za mijini hasa ikizingatiwa zina vifaa na miundo misingi bora zikilinganishwa na zile mashambani,” aeleza Prof Bekele.
Kwa wagonjwa wa mashambani, Dkt Kabetu aeleza, gharama za usafiri, safari ndefu na ukosefu wa vifaa hospitalini husababisha vifo katika sehemu hizi.
Kwa hivyo ni nini kimechangia tatizo la uhaba wa wataalam wa upasuaji barani? Kulingana na Dkt Bekele, tatizo kuu limekuwa uhamaji wa wataalamu.
“Wahudumu walio na ujuzi wa juu hapa Afrika wanaendelea kutafuta kazi ughaibuni, sio tu kwa sababu ya pesa, bali pia, mazingira duni ya utendakazi,” aeleza Dkt Stephen Okelo, mtaalam wa unusu kaputi na mkufunzi katika shirika la Global Heart Association.
Kwa mfano, kulingana na utafiti ulichapishwa Januari 2023 katika jarida la Global Public Health Journal, kati ya mwaka wa 2008 na 2021, takriban madaktari 35,000 waliondoka nchini Nigeria na kuhamia nchini Uingereza pekee.
Kwa wahudumu, idadi inasikitisha hata zaidi kwani kati ya mwaka wa 2002 na 2021, zaidi ya wahudumu 60,000 kutoka nchini humo walihamia nchini Uingereza.
Nchini Kenya, ripoti ya mwaka wa 2023 kutoka kwa Wizara ya Afya ilionyesha kwamba asilimia 64.4 ya wahudumu wa afya walionyesha nia ya kuondoka humu nchini.
Madaktari na wataalam wa kimatibabu wanasisitiza kwamba ili kukabiliana na janga la uhaba wa wataalam wa upasuaji barani, sharti suala la muundo msingi na teknolojia liangaziwe.
“Lazima serikali za Afrika ziwekeze kiwango kikubwa cha pesa katika teknolojia, miundomisingi na mafunzo kwa wahudumu,” aeleza Dkt Okelo.
Bi Kathy Magee, mwanzilishi mshirika wa shirika la Operation Smile, ambalo limekuwa likitoa huduma za upasuaji katika mataifa kadhaa barani, anasema sharti serikali za Afrika ziungane na mashirika ya kimataifa na jamii. “Hili sio tatizo ambalo laweza kutatuliwa na mtu mmoja,” aongeza.
Lakini kando na masuala haya, Dkt Bekele asema ni wakati wa mifumo ya mafunzo ya udaktari barani kubadili mienendo. Kulingana na Dkt Bekele, katika mataifa mengi hapa barani, mifumo ya mafunzo ya udaktari inaendeleza ubaguzi uliokuwa ukitekelezwa na wakoloni.
“Katika enzi za kikoloni, ubaguzi wa rangi ulitumika kuwachagua wale walioruhusiwa kusomea udaktari na kufuzu, suala lililowatenga watu weusi. Kinachohuzunisha ni kwamba hata sasa kuna Waafrika wanaoendeleza mifumo hiyo ya kibaguzi kuamua nani atakayejifunza udaktari na kufuzu,” aeleza Prof Bekele, huku akiongeza kuwa hiki kimekuwa kizingiti katika jitihada za kuongeza idadi ya wataalam katika nyanja hii barani.