Nitakuwa debeni katika kura za urais 2027 -Karua
KIONGOZI wa Chama cha People’s Liberation Party, Martha Karua, amesema hatakuwa mgombea mwenza katika uchaguzi wa urais wa 2027.
Akizungumza wakati wa majadiliano katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Nation Media Group katika Klabu ya Gofu ya Muthaiga jijini Nairobi Ijumaa, Bi Karua alisema kuwa analenga kushinda kiti baada ya kugombea kama mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022.
“Nataka kuwa rais, na nitagombea,’ alisema Bi Karua huku akifafanua uzoefu wake wa kisiasa wa awali akiwa mgombea mwenza wa urais na gavana.
Hata hivyo, alisema kuwa wakati ufaao utakapofika wa muungano ambao atashiriki kufanya uamuzi, atauheshimu kwa kuwa ‘Kenya ni kubwa kuliko mimi.’
Mbunge wa Suba Kaskazini, Millie Odhiambo, ambaye pia ni Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, alisema mazingira ya kisiasa mara nyingi huwaacha wanawake nje ya maamuzi muhimu.
Alisisitiza haja ya kutekeleza sheria za usawa, kama vile sheria ya theluthi mbili ya kijinsia, na sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia (GBV). Alisema kwamba hata ingawa sheria kama hizo zipo, utekelezaji wake umesalia kuwa changamoto.
“Wanawake tunakabiliwa na changamoto tofauti za kisiasa. Lakini tunapoungana, tunaweza kuleta mabadiliko ya kudumu,” alisema Bi Odhiambo, akihimiza mshikamano wa wanawake katika siasa.
Bi Faith Odhiambo, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), alielekeza mjadala kwenye suala la dharura la ukatili wa kijinsia nchini Kenya, akitoa wito wa mageuzi ya haraka ya mahakama ili kushughulikia ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake na ukatili dhidi ya wanawake.
Alisisitiza hitaji la kuongezwa kwa ufadhili wa Idara ya Mahakama, akitaja tofauti katika mgao wa bajeti ikilinganishwa na mihimilj mingine ya serikali, kama vile Bunge na Serikali Kuu.’Hauwezi kusema hakuna pesa za kutosha kwa mahakama ilhali tunaona fedha zinazotengewa Bunge,’ alisema.