Ruto, Raila kuvumisha muafaka wao Nairobi wiki mzima

0

RAIS William Ruto amepanga misururu ya mikutano ya kisiasa Nairobi wiki hii kuvumisha muafaka kati yake na Kinara wa Upinzani Raila Odinga uliotiwa saini Ijumaa iliyopita.

Bw Odinga anajivunia ufuasi mkubwa katika siasa za jijini na Rais Ruto anatarajia kutumia ushirikiano huo mpya kupenya Nairobi. Bw Odinga ana idadi ya juu ya wabunge na madiwani ikilinganishwa na UDA Nairobi.

Rais anatarajiwa kuzindua barabara, hospitali, miradi ya taa na shule akikutana na viongozi wa ODM na UDA mashinani kuvumisha ushirikiano wake na Bw Odinga.

Mkuu wa Mawasiliano ya Rais Munyori Buku alithibitisha ziara hiyo ambayo alisema ni ya maendeleo lakini hakufafanua miradi ambayo itazinduliwa na Rais.

Bado haijafahamika iwapo Bw Odinga ataungana naye kwenye ziara hiyo ila wabunge wake wameamrisha waandamane na Rais anayeanza ziara hiyo eneobunge la Kamukunji.

Ziara hiyo inaonekana kama itakayochemsha siasa za Nairobi hasa zile za ugavana ambazo zinawaniwa na ODM na UDA. Inakuja baada ya Bw Odinga wiki jana kuonekana kumpigia upato Gavana Johnson Sakaja kutetea wadhifa wake mnamo 2027.

Mbunge wa Kibra Peter Orero na mwenzake wa Makadara George Aladwa Jumapili waliambia Taifa Leo kuwa maeneobunge yao yameorodheshwa kwenye ziara ya rais ambapo serikali ya kitaifa itazindua miradi ya maendeleo.

“Atazindua madarasa 13 Ayany, taa kwenye barabara za Kibra kisha aweke jiwe la msingi kwa ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo na Chuo cha Ufundi pamoja na miradi mingine,” akasema Bw Orero.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiri maarufu kama MejjaDonk, mwandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua naye alisema hana habari kuhusu ziara hiyo.

“Sina habari na kama ni miradi, hakuna mradi wowote serikali ya kitaifa imefanya katika eneobunge langu ambao utazinduliwa. Kile tuko nacho ni madarasa ambayo yalijengwa na fedha kutoka Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF),” akasema Bw Gathiru.

Bw Sakaja alisema kuwa muafaka wa Rais na Bw Odinga ni muhimu kwa sababu sasa mazingira ya kisiasa ni tulivu na kilichosalia ni miradi kukumbatiwa moja baada ya mingine.

Gavana huyo alisema pia ziara hiyo inalenga kufuatilia mahali ahadi ya rais ya kujenga madarasa 5,000 imefika. Wabunge wa Nairobi walipewa ahadi hiyo mwaka jana na Bw Sakaja anasema ujenzi wa madarasa hayo umekamilika.

“Pia tutakuwa tukisikiza kile wafuasi wa ODM na UDA watasema kwenye mikutano yao. Kumbuka mwaka jana, tulimshinikiza Rais atoe Sh1 bilioni zaidi kwa ujenzi wa madarasa Nairobi,” akasema.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *