Hamtanipanga, asema Ruto akitoa sadaka nyingine ya Sh20 milioni licha ya maandamano
SADAKA ya Rais William Ruto Jumapili iliendelea kuchafua hewa baada ya maafisa wa polisi kupambana na vijana waliojaribu kuvamia kanisa ambako kiongozi wa taifa alitoa Sh20 milioni wiki jana kufadhili miradi.
Rais Ruto akiwa Kaunti ya Uasin Gishu aliwapuuzilia mbali vijana hao na watu wanaopinga matoleo yake makanisani huku akitoa Sh20 milioni za kufadhili ujenzi wa jengo jipya la Kanisa ya AIC Fellowship Annex, Eldoret.
Aliapa kwamba vijana hawatapanga kuhusu matoleo yake makanisani akiapa kuendelea kujenga nyumba ya Mungu.
“Mimi sitatishwa na watu wa mitandao, nitaendelea kujenga makanisa lakini sijasema wasipende, la mno ni kwamba sharti tujenge makanisa,” Dkt Ruto akaeleza.
Jana, zaidi ya vijana 10 walijeruhiwa kwenye makabiliano kati yao na polisi walipojaribu kuvamia Kanisa la Jesus Fellowship Ministry wakitaka Sh20 milioni ambazo Rais Ruto alidaiwa kumpa kiongozi wa Kanisa hilo Askofu Edward Mwai Jumapili, Machi 2, 2025.
Vijana hao walipinga mchango huo wakisema ni kinyume na agizo lake (Rais Ruto) la kupiga marufuku maafisa wa serikali kutoa michango ya fedha makanisani.
Rais alitoa agizo hilo, baada vijana kufanya maandamano ya kuipinga serikali mwaka jana, kama njia ya kuzuia ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Jana asubuhi Gen Zs walikongamana katika eneo la Roysambu, tayari kuandamana hadi katika Kanisa la Jesus Winner Chapel lakini wakazuiliwa na polisi waliowatawanya kwa kuwarushia vitoza machozi.
Aidha, vijana ambao walifaulu kuingia ndani ya Kanisa hilo, lililoko katika barabara ya Thika Mall Drive, kabla ya saa tatu za asubuhi, walinaswa na polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia wakijifanya kuwa waumini.
Walizabwa makofi mara kadhaa kisha wakarushwa kwenye malori na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kasarani.
Vijana wengine hawakufa moyo kwani walikongamana katika Mzunguko wa Barabara ya Roysambu na kuanza kukabiliana na maafisa wa polisi.
Waliwarushia maafisa hao mawe na vijiti ambao walijibu kwa kurusha vitoza machozi zaidi kuwatawanya wasivamie kanisa hilo.
Makabiliano hayo yalidumu kwa saa kadhaa na kuchangia vijana kadhaa kujeruhiwa.
Waandaamanaji hao walitoa kauli za “Ruto Must Go” (Ruto Lazima Aende), wakati wa makabiliano hayo.
Baada ya vijana hao kung’amua kuwa hawangefaulu kuvamia Kanisa hilo na kuvuruga ibada, walielekeza hamaki zao katika Barabara Kuu ya Thika.
Waliziba barabara hiyo kwa miamba, wakiteketeza magurudumu na kuvuruga shughuli za usafiri katika barabara hiyo yenye magari mengi.
Bw John Isaboke, ambaye ni mkazi wa Roysambu na mfanyabiashara katika barabara ya Thika Road Mall Drive, alisema anaunga mkono hatua ya vijana “kwa sababu wanapigania uwajibikaji katika matumizi ya pesa za umma.”
“Mbona Rais alitoa mchango wa Sh20 milioni kwa kanisa ambalo ujenzi wake umekamilika ilhali maelfu ya Wakenya wanakosa huduma muhimu za afya na maji?” akauliza.
Naye John Gichana alisema mpango wa vijana “kuvamia” Kanisa la Jesus Winner Ministry ni ishara kwamba Wakenya wamechoka kuchezewa shere na wanasiasa ambao hawayapi uzito masuala yanayowahusu na badala yake “wanaelekeza pesa katika mambo yasitufaidi.”
“Hatuwezi kukaa kitako na kutazama Rais akipeana mamilioni ya pesa kwa wandani wake wakati ambapo mamlaka ya afya ya kijamii (SHA), mfumo wa ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu na mpango wa ufadhili wa masomo shule, hayafanyi kazi,” akasema.
Lakini akisema Eldoret, Rais Ruto alikariri kuwa hamna anayepaswa kumzuia kutoa michango makanisani, akisema matoleo yake yanalenga kufanikisha kazi ya Mungu.
“Natoa kwa nyumba ya Mungu ili kupambana na uraibu wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na ili kanisa itekeleze wajibu wake wa kupalilia maadili miongoni mwa vijana,” akawaambia waumini katika Kanisa la AIC Fellowship, Annex, lililoko eneo bunge la Kesses.
Dkt Ruto aliwataja wanaopinga matoleo yake kama maajenti wa shetani aliosema kuwa watashindwa kwa nguvu za Mungu.
“Shetani amekuwa mjeuri zaidi nchini Kenya. Ningependa kutaja hilo, kama Rais wa Kenya na kwa Neema ya Mungu, kama kiongozi wa taifa. Bibilia inatuambia katika Kitabu cha Danieli 11: 32 kwamba wale wanaojua Mungu watapata nguvu na kufanya makuu. Nataka kusema kuwa Kenya itamjua Mungu, na tutafanya makuu,” Dkt Ruto akaeleza.