Raila alivyokutana ana kwa ana na ghadhabu za Wakenya Kisii

0

KINARA wa ODM Raila Odinga Jumapili alikumbana na ghadhabu za Wakenya ambao hawajafurahishwa na hatua yake ya kuhalalishwa uhusiano wake wa kisiasa na Rais William Ruto.

Siku mbili tu baada ya kutia sahihi mkataba wa kisiasa na Rais Ruto, mwanasiasa huyo mkongwe, jana alizomewa vikali na vijana alipojiunga nao katika kaunti ya Kisii.

Haya yalikuwa kwenye hafla ya uzinduzi wa sare mpya za timu ya Shabana, inayoshiriki ligi kuu ya kitaifa (FKF-PL) katika uga wa Gusii.

Vijana hao walimpigia mayowe Bw Odinga kwa kipindi kirefu alichokuwa uwanjani humo, wakitoa kauli za “Ruto Must go! Raila must go!”

Mashabiki hao pia walisikika wakiliimba jina la aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, anayesemekana kumezea mate kiti cha urais katika kinyang’anyiro cha 2027.

Sherehe iliyopambwa kwa kila aina ya mbwembwe na madoido ilibadilika tu ghafla pale mshereheshaji wa siku alipotambua uwepo wa Bw Odinga uwanjani.

Kiongozi huyo wa ODM alikuwa ametua uwanjani humo dakika chache tu kabla ya saa nane mchana akiwa ameandamana na magavana Johnson Sakaja (Nairobi), na Ochilo Ayacko (Migori).

Walipokelewa na mwenyeji wao gavana Simba Arati. Baada ya hapo viongozi hao walielekea kwenye ukumbi wa watu mashuhuri uwanjani humo ambapo walifanya kikao kifupi.

Walitoka kwenye ukumbi huo wakiwa wamevalia jezi nyeupe za Shabana, zenye michirizi mieusi, zenye jina la kampuni ya michezo ya kamari ya Sportpesa, ambao ndio wadhamini wakuu wa Shabana. Waliingia uwanjani na kucheza mpira kidogo kabla ya kurudi kwenye jukwaa kuu kwa sherehe.

Mara Bw Odinga alipochukua kiti chake katika eneo hilo, mshereheshaji aliutambua uwepo wa Bw Odinga kwa kulitaja jina lake na hapo maji yalianza kuzidi unga.

Vijana wakizua rabsha uwanja wa Gusii wakilalamikia Raila kushirikiana na Rais William Ruto. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Ruto Must Go! Raila Must Go!” Vijana hao waliimba huku wakipunga mikono kwa pamoja. Wengine walirusha viti vya plastiki hewani huku wengine wakitaja jina la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, anayetoka eneo hilo.

Hali hiyo ilileta hali ya taharuki uwanjani.

Wale waliohofia maisha yao walilazimika kukimbia kwa usalama wao huku walinda usalama wakijibidiisha kutuliza hali.

Vijana hao walimkashifu waziri mkuu huyo wa zamani kwa matamshi aliyoyatoa wiki jana kumhusu Bw Matiang’i alipozuru kaunti ya Kisii.

Alhamisi wiki jana, Bw Odinga, alikutana na wajumbe kutoka kaunti za Kisii na Nyamira, siku moja kabla ya kutia saini mkataba wa kisiasa na Rais William Ruto.

Baada ya kufanya kikao na wajumbe hao, alipuuzilia mbali azma ya Dkt Matiang’i ya kutaka kuingia Ikulu akisema kuwa Waziri huyo wa zamani hawezi kuwa Rais kwa kura ya Abagusii pekee.

“Tumemuunga mkono kwa muda mrefu. Kwa nini alitoa matamshi kama haya. Kila mgombea Urais ana jamii anayotoka. Kwa nini basi kuleta suala la jamii anapokuja kwa Dkt Matiang’i? Tulisikitishwa na hisia zake ambazo zilionekana kutudharau (Abagusii),” shabiki mmoja alisikika akisema.

Gavana wa Kisii, Simba Arati na seneta wa Migori Eddy Oketch nao pia walipata wakati mgumu kuhutubu walipojaribu kutuliza umati huo mkubwa ulioujaza uwanja huo.

Gavana Arati alitumia lugha ya mama kujaribu kuwashawishi vijana hao kuwa watulivu lakini hayo yalianguka kwenye masikio ya yasiyosikia.

“Acha niwaambie, hivi sivyo tunavyopaswa kufanya. Hata ikiwa tuna mtu kutoka kwa jamii yetu anayetazama kiti hicho, hivi sivyo tunavyopaswa kuwarai watu wengine ambao tunataka watuunge mkono. Tafadhali tulieni,” Gavana Arati alirai kwa Ekegusii

Bw Odinga aliposimama kuzungumza, kelele ziliongezeka zaidi. Vijana hao walimkashifu kwa kuungana na Rais Ruto wakisema amewasaliti.

Wengine walianza kuondoka uwanjani lakini mwanasiasa huyo mkongwe alijibidiisha na kutoa hotuba fupi.

Bw Odinga alisema tayari ameamua kushirikiana na Rais Ruto kuunganisha nchi na kupambana na ufisadi ambao alisema unaiangamiza nchi hii.

“Mimi ndiye Raila moja. Tumekubaliana kutembea na kufanya kazi pamoja. Yule anayesema ng’we ng’we, shauri yake,” Odinga akafoka.

Kiongozi huyo wa ODM, ambaye alirejea katika siasa za nchi baada ya kupoteza Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) alisema atarejea Kisii kuzungumza na wafuasi wake.

Kwa miaka mingi, eneo la Gusii limemuunga mkono Bw Odinga kwa nia zake kadhaa zilizofeli za kuwania Urais.

“Nitarudi hivi karibuni kuzungumza nanyi watu wangu. Mmeniunga mkono kwa muda mrefu,” Bw Odinga alisema na kisha kupeana kipaza sauti.

Alikumbuka safari ya Shabana kutoka mashinani hadi kurejea ligi ya premia na kusema atasaidia timu hiyo.

Alitoa mchango wa Sh1 milioni kwa timu hiyo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *