Kituo cha data Naivasha kilichofyonza Sh2 bilioni za walipa ushuru bado hakifanyi kazi

0

MRADI wa serikali wa ujenzi wa kituo cha kitaifa cha kuendesha shughuli za ukomboaji wa data, mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru wa gharama ya Sh2 bilioni haujafaidi walipa kodi.

Baada ya zaidi ya mwongo mmoja, mradi huo ulioanzishwa mnamo 2009, haujaanza kufanya kazi huku gharama yake ikiendelea kuongeza na kuibua hofu kuhusu matumizi mabaya ya pesa za umma.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu wa mwaka wa kifedha wa 2023/2024 inaonyesha kuwa Hazina ya Kitaifa ilianzisha mradi huo ili kuunda hifadhi ya data zitakazotumiwa na serikali.

Kandarasi ilitolewa kwa kampuni moja kwa gharama ya Sh782 milioni, huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika ndani ya wiki 96.

Hata hivyo, baadaye mradi huo ulipanuliwa na kugawanywa kwa awamu tatu.

Awamu ya kwanza iligharimu Sh899 milioni, ilhali awamu ya pili iligharimu Sh205 milioni. Miradi hiyo miwili ilikamilishwa na kulipiwa na hivyo asilimia 68 ya kazi zote zikiwa zimekamilishwa.

Hata hivyo, mvutano kuhusu malipo katika awamu ya tatu ulikwamisha mradi huo na kupelekea hasara zaidi kifedha.

“Hali ya kutoelewana ilitokea baada ya Hazina ya Kitaifa kufeli kulipa Sh193 milioni zilizosemekana kuwa fidia kwa rasilimali zisizotumika na kucheleweshwa kwa ukamilishaji wa kazi. Mwanakandarasi aliwasilishwa suala hilo mbele ya jopo la utatuzi mizozo ambalo liliagiza alipwe Sh4.1 bilioni ‘kupoteza faida na gharama nyinginezo,’” ripoti hiyo ya Bi Gathungu inasema.

“Kufikia Juni 30, 2024, madeni yaliongezeka hadi Sh5. 5 bilioni kutokana na riba. Ingawa uamuzi wa jopo la kutatua mizozo uliidhinishwa na Mahakama ya Kuu na mwanasheria mkuu akaonyesha dalili za ufanisi endapo kesi ya rufaa ingewasilishwa ilikuwa finyu na Hazina ya Kitaifa ikaagizwa ielewane na mwanakandarasi, hakuna ushahidi uliowasilishwa kwamba mazungumzo yalifanyika,” ripoti hiyo inaendelea kusema.

Hazina ya Kitaifa ilidai kuwa awamu ya tatu ya mradi huo ilikuwa tenda tofauti iliyohitaji mpango mpya wa maelewano.

Hata hivyo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amelaumu maafisa wa Hazina ya Kitaifa kwa usimamizi mbaya wa kandarasi hiyo.

Bi Gathungu anasema mzigo huo wa kifedha ungeepukwa endapo kungekuwa na usimamizi mzuri wa pesa za umma.

“Pesa zilizotumika zingeokolewa endapo Hazina ya Kitaifa ingezingatia sheria na kanuni hitajika wakati wa utoaji wa zabuni hiyo,” Bi Gathungu akasema.

Mkaguzi huyo pia alisema kuwa jengo hilo bado halitumiki na hivyo kuashiria ubadhirifu wa pesa za serikali katika miradi.

“Katika hali hiyo, thamani ya Sh1,987, 278,191 haingeweza kuthibitishwa. Kulipwa kwa pesa hizo kutaathiri bajeti ya wizara ya fedha na hivyo hakufaidi umma,” Bi Gathungu akaeleza.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *