MAONI: Raila si msaliti, wakosoaji wake pia wana fursa kujaribu upinzani
KINARA wa upinzani Raila Odinga hajamsaliti mtu yeyote baada ya kuingia kwenye muafaka na Rais William Ruto kwa sababu alifanya hivyo kuhakikisha taifa linasalia dhabiti na linadumisha umoja.
Mnamo Ijumaa wiki jana, waziri huyo mkuu wa zamani na Rais Ruto walijitokeza hadharani na kurasimisha uhusiano wao na yaliyomo kwenye mkataba huo, yatawafaa Wakenya iwapo watamakinikia kuyatekeleza.
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa na Wakenya wasiokuwa na mwao kuhusu utaifa na kuweka kando maslahi ya kisiasa, wamekuwa wakikesha mitandaoni wakimtusi Raila na kumrejelea kama mwanasiasa msaliti ambaye anajaza tu tumbo lake kwa kushirikiana na Rais.
Mwanzo, ni wazi kwamba Raila Odinga katika taifa hili ni mwanasiasa mtelezi sana.
Hii ni kwa sababu hata wapinzani ambao hawakumpigia kura, waliomtusi, wakamrejelea kama mkabila, wana ujasiri wa kukashifu na kutaka uwapiganie dhidi ya serikali waliyoichagua kisha ikawageuka.
Huu utawala wa Rais Ruto ulikuwa malaika na ulipigiwa kura na Wakenya hasa kutoka Mlima Kenya ambao sasa wanaongoza katika kumkashifu Bw Odinga mitandaoni na kudai kuwa amesaliti nchi.
Ni kweli taifa haliko mahali pazuri kutokana na changamoto mbalimbali za kiuchumi ila hawa wanaopiga kelele ndio walihakikisha kuwa Rais Ruto ameingia mamlakani.
Wakati ambapo Raila alikuwa akiendeleza mapambano dhidi ya serikali baada ya uchaguzi wa 2022, hawa wanaosema yeye ni msaliti ndio walikuwa wakisema anataka uongozi kupitia mlango wa nyuma.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na wafuasi wake ambao sasa wanamwona Bw Odinga kama adui, ndio walikuwa mstari wa mbele kudai asingeingia kwenye serikali ambayo hakupigania na kuunga ukatili wa serikali dhidi ya wafuasi wake.
Inakuwaje kwamba sasa wao ndio wapo mstari wa mbele kumkashifu Raila, kumrejelea kama msaliti na kusema anaunga utawala dhalimu?
Wao ndio walimuunga Rais Ruto 2022. Je, kuna kosa gani Raila kumuunga mkono mtu waliyemvumisha na akafaulu uchaguzini?
Pili, upinzani haukuumbiwa familia ya Bw Odinga pekee. Kuna wanasiasa wengi na wenye maoni kinzani wanaoweza kuendeleza maasi dhidi ya serikali kupigania utawala wa bora.
Zawadi ambayo Raila angepewa kwa kupigania demokrasia, uhuru wa kujieleza na kuzima udikteta nchini ni kuchaguliwa rais.
Lakini hawa hawa wanaomlaumu walikataa kumchagua 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022 ilhali wanataka awatumikie katika upinzani hata akiwa na ukongwe wa miaka 80.
Ufuasi wa kisiasa ambao kiongozi huyo wa ODM amejivunia nchini haukuja kwa urahisi. Ulitokana na misimamo na maamuzi magumu ya kisiasa.
Wale wanaomkosoa nao pia wajitume, watafute wafuasi ili wadhibiti nchi kisiasa jinsi ambavyo Bw Odinga amekuwa akifanya.
Kama ni maandamano, silazima Raila ayaongoze! Wanaomkosoa kwa sasa waende pia barabarani.
Ukombozi wa taifa huwahitaji Wakenya wote wala si Raila pekee kwa sababu matunda yake nayo huwanufaisha watu wote.
Kwa viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa na Bw Gachagua, hakuna haja ya kukesha usiku na mchana wakimkiponda Raila kwa kufanya kazi na Rais Ruto.
Kile ambacho wanasiasa hawa wanastahili kumakinikia ni mikakati ambapo wataibuka na mwaniaji bora ambaye atambwaga Rais Ruto mnamo 2027.