Sudi aondolea kesi Gen Z waliovamia na kuiba katika kilabu chake cha Timba XO
NI afueni kwa vijana 16 wa Gen Z ambao wamekuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuiba mali ambayo ilikuwa ni pamoja na vifaa pombe na kuharibu mali nyingine yote ya kima cha Sh150 millioni, mali ya Timba XO Club inayohusishwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.
Vijana hao wanaodaiwa kushiriki uhalifu huo wakati wa maandamano ya Gen Z mwezi Juni mwaka jana wameondolewa mashtaka na mahakama ya Eldoret baada ya Bw Sudi kupitia kwa meneja wa klabu hiyo kuwasilisha ombi la kuondoa kesi na kusamehe washtakiwa wote.
Hapo Jumanne wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya hakimu mwandamizi wa Eldoret Cheronoh Kesse, mahakama iliambiwa kuwa mbunge huyo hakuwa na nia ya kuendelea na kesi husika dhidi ya washtakiwa.
“Ikizingatiwa kuwa mlalamishi ametangaza kuachana na kesi hii, sina jingine ila kuondolea mbali mashtaka yote dhidi ya washtakiwa,” alisema hakimu huku akifunga faili ya mashtaka hayo.
Mamia ya jamaa ya washtakiwa ambao walikuwa wamefurika mahakamani walishangilia uamuzi huo kwa nyinbo za kushukuru Mungu na mbunge huyo kwa hatua hiyo.
Vijana hao ambao walikuwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati walidaiwa kutekeleza uhalifu huo wakati wa maandamano ya Gen Z mjini Eldoret mnamo Juni 25 ambapo walivunja kilabu hicho na kuiba mali hiyo wakati wa maandamano.
Stakabadhi za mashtaka mahakamani zilionyesha kuwa, washtakiwa waliiba spika 11, runinga, vipakatalishi, vifaa vya jikoni, mitungi ya gesi, pombe miongoni mwa mali nyingine yenye thamani ya Sh78,896,560 yote ikiwa mali ya Timba XO Lounge.
Vile vile, walikabiliwa na mashtaka mengine ya kuharibu mali ikiwa ni pamoja afisi, kamera za CCTV, pombe, fanicha vifaa meme miongoni mwa mali nyingine ya kima cha Sh80 milioni.
Washtakiwa wengine walikabiliwa na mashtaka ya kupatikana mali ya wizi.
Kwa pamoja walikana mashtaka husika dhidi yao.
Tangu wafikishwe mahakamani mwezi Julai 2024 baadhi yao wamekuwa katika rumande ya jela kuu ya Eldoret baada ya kushindwa kumudu dhamana ya Sh200,000 kila mmoja.