Raila: Watu wanapiga kelele kwamba nilitafuta Ruto ilhali ni yeye alinifuata

0

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, Jumanne alitetea uamuzi wake wa kutia saini mkataba wa ushirikiano na Rais William Ruto, akifichua kuwa ni Rais mwenyewe aliyemsaka amsaidie.

Bw Odinga alisema kuwa uamuzi wake wa kushirikiana na Rais Ruto ulilenga kumpa nafasi ya kutoa suluhisho kwa changamoto zinazokumba nchi, akisisitiza kuwa mtu anaweza kurekebisha mambo akiwa ndani na si kwa kupiga kelele akiwa nje.

Alifichua haya wakati wa mazishi ya marehemu Kimani Waiyaki huko Muthiga, Kaunti ya Kiambu, akieleza wasiwasi wake kuhusu changamoto zinazokumba mpango wa huduma ya afya kwa wote wa Rais Ruto.

“Watu wengi wanapiga kelele hapa na pale wakisema nilimfuata Ruto; kwamba Raila amemfuata Ruto na kutuacha. Sikumfuata Ruto, ni Ruto ndiye aliyenitafuta,” alisema Bw. Odinga.

“Nafasi yangu kuhusu masuala ya kitaifa haijabadilika. Katika maisha yangu yote, nimekuwa nikisimama kwa ukombozi na ustawi wa wananchi. Mnajua kwamba mnamo 2023 tuliandamana  kupinga gharama kubwa ya maisha. Wakenya walisema kuwa gharama ya maisha ilikuwa mzigo kwao,” aliongeza Bw Odinga.

Aliibua wasiwasi kuhusu utekelezaji duni wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) kutokana na mfumo wake kuwa na hitilafu, hali iliyopelekea malimbikizi ya madeni ya matibabu hadi mabilioni ya pesa.

“Nimemwambia Ruto kwamba SHA ina matatizo na inapaswa kurekebishwa. Ushuru unaowekewa Wakenya pia ni wa juu sana, hasa wa nyumba,” alisema Bw Odinga.

“Mambo haya hayawezi kurekebishwa ukiwa nje, lazima uingie ndani na kuwaambia cha kufanya. Na lazima uweke watu mahali hapo kushughulikia matatizo hayo,” aliongeza Bw  Odinga.

Bw Odinga amekosolewa na umma kufuatia mkataba wakena Dkt Ruto. Jumapili alizomewa katika Kaunti ya Kisii, jambo ambalo limefichua hatari ya kisiasa na upinzani anaoweza kukumbana nao kwa kushirikiana na Rais Ruto, ambaye serikali yake inakabiliwa na uhasama mkubwa kutokana na ahadi zilizotekelezwa na sera zisizopendwa na wananchi.

Kwa kushirikiana na Rais Ruto, Bw Odinga anajiweka katika hatari ya kubebeshwa mzigo wa utawala wa Kenya Kwanza, anayelaumiwa kwa kushindwa kutimiza ahadi zake, kama vile kuunda nafasi za kazi kwa vijana wasio na ajira na kutopatia kipaumbele mahitaji ya wananchi wa kipato cha chini.

Bw Odinga hapo awali alikuwa akiikosoa serikali kwa kuongeza ushuru, hali ambayo imesababisha Wakenya walioajiriwa kupokea mishahara isiyokidhi mahitaji yao.

Ushuru wa Nyumba, ambao umesababisha mishahara kushuka zaidi, pia haujawapendeza Wakenya wengi.

Kwa kushirikiana na Rais Ruto, Bw Odinga anaweza kuwekwa kwenye kundi moja na utawala wa Kenya Kwanza kwa sababu ya ahadi ambazo hazijatimizwa, pamoja na sera ambazo zimeendelea kuwaumiza wananchi wa kawaida. Uamuzi wake unaweza kumfanya apoteze baadhi ya wafuasi wake wa jadi, hususan katika maeneo ambayo yamekuwa yakimuunga mkono kwa miaka mingi kutokana na misimamo yake thabiti na maono yake ya kuiboresha nchi.

“Inahuzunisha sana kuona Mheshimiwa Raila Amollo Odinga akizomewa na umma katika Nyanza. Kuzomewa huko ni ishara ya wazi ya hasira za wananchi dhidi ya utawala wa Ruto na kila kinachohusiana nao,” alisema Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, mshirika wa kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *