Ni kunyamazishwa? Mdhibiti wa Bajeti alalamikia ofisi yake kupunguziwa mgao

0

MDHIBITI wa Bajeti, Margaret Nyakang’o, ameonya kuwa shughuli za ofisi yake huenda zikakwama kufuatia kupunguzwa kwa bajeti yake kwa Sh850 milioni katika mwaka ujao wa kifedha.

Hatua hii inajiri wakati ambapo Dkt Nyakang’o ameanika maafisa wa serikali ya kitaifa kwa kukwepa makusudi mfumo uliowekwa ili kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za walipa kodi.

Bi Nyakang’o alisema kwamba licha ya kuwepo kwa mfumo wa kidijitali ambao unafanya kazi kikamilifu, wizara, idara na mashirika ya serikali bado zinaendelea kufanya maombi ya matumizi ya fedha nje ya mfumo huo, huku wakitumia mfumo huo kwa nadra na kwa uchaguzi mara kwa mara.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti jana, Mdhibiti wa Bajeti alisema kuwa Sh704.25 milioni ambazo ofisi yake ilipokea kwa mwaka wa sasa wa kifedha zimeisha.

Aliambia kamati inayoongozwa na Seneta wa Mandera, Ali Roba, kwamba kwa sasa wanategemea kupata fedha kutoka kwa bajeti ya pili ya nyongeza ili waweze kufanikisha shughuli zao hadi mwisho wa mwaka wa kifedha.

Dkt Nyakang’o alisema kuwa shughuli muhimu kama vile ufuatiliaji na tathmini, utayarishaji wa ripoti, kujenga uwezo, mijadala ya utekelezaji wa bajeti na safari za ndani za kikazi zimekwama baada ya bajeti yao kuisha.

Alifafanua kuwa ufuatiliaji na tathmini, ambao ulikuwa na bajeti ya Sh28.9 milioni, tayari umekwama, sawa na uhamasishaji wa umma na safari za ndani za kikazi.

“Tuna bajeti ndogo sana na tunaendelea tu kwa sababu tumepunguza matumizi yetu hadi kiwango cha chini kabisa,” alisema Dkt Nyakang’o.

Aliongeza kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika mwaka wa kifedha unaoishia Juni 2026, kwani Serikali ya Kitaifa imetenga kiasi cha Sh777.5 milioni pekee kwa ofisi yake, licha ya wao kuomba Sh1.63 bilioni.

Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizomo kwenye taarifa ya sera ya bajeti, ofisi yake itakumbwa na upungufu wa Sh855.96 milioni.

Dkt Nyakang’o alieleza kuwa kupunguzwa kwa bajeti kutanyima ofisi yake fedha za kutosha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.Alibainisha kuwa maeneo tisa ya kipaumbele katika utendakazi wake yamekumbwa na upungufu wa Sh579.3 milioni, jambo ambalo linaashiria changamoto kubwa kwa ofisi yake.

“Tumetengewa chini ya asilimia 50 ya kile tulichoomba, na itakuwa kazi ngumu kufanikisha malengo yetu,” alisema Dkt Nyakang’o.

“Tunaiomba Seneti iingilie kati na kututengea angalau Sh579.3 zaidi milioni katika mwaka ujao wa kifedha ili kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi. Bila ufadhili huu, tuko kama gari lililokwama,” aliongeza.

Kwa mfano, alisema waliomba Sh182.8 milioni kwa mwongozo wa maendeleo ya kazi lakini hawakupatiwa chochote, sawa na Sh102 milioni zilizokusudiwa kwa mapendekezo ya sheria ya kuimarisha shughuli za ofisi yake.

Vile vile, waliomba Sh50 milioni kwa uboreshaji wa mifumo ya kidijitali lakini hawakupatiwa hata senti moja, sawa na Sh24 milioni za kujenga uwezo na Sh15.3 milioni kwa safari za nje ya nchi.

“Tangu nilipojiunga na ofisi hii miaka sita iliyopita, sijawahi kusafiri nje ya nchi kujifunza mbinu bora. Ofisi yangu pia imekuwa ikipoteza wafanyakazi wengi, ambapo saba wameondoka ndani ya miezi sita iliyopita kutokana na mishahara duni. Maafisa wangu wamekata tamaa,” alisema.

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alimweleza Dkt Nyakang’o kuwa wanatambua changamoto zake na watahakikisha ofisi yake inapata fedha za kutosha.

“Kwa miaka mitatu iliyopita umekuwa ukililia ufadhili zaidi ili kusaidia kulinda fedha za umma lakini hakuna kilichofanyika. Tutahakikisha tunakupa nyenzo za kufanya kazi yako ya kupambana na ufisadi nchini,” alisema Seneta wa Kisii, Richard Onyonka.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *