Siri ya kujaza kibaba katika ufugaji nyuki

0

ERICK Kamau na mwasisi mwenza Waiyaki Way Beekeepers, Philip Muchemi, wamekuwa kwenye ufugaji wa nyuki kwa zaidi ya miaka mitano.

Ni kampuni ya bidhaa zinazotokana na ufugaji nyuki iliyozinduliwa 2019, na kuanza rasmi huduma zake mwaka wa 2020, janga la corona liliposhuhudiwa Kenya na kwengineko ulimwenguni.

Kilikuwa kipindi ambacho asali – mojawapo ya mazao ya nyuki, ilikuwa inasakwa sana.

“Asali ina manufaa mengi kiafya, na 2020 wengi waliisaka kuitumia pamoja na mimea asilia kuzima makali ya Homa ya virusi vya corona,” Muchemi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Waiyaki Way Beekeepers anasema.

Kamau ndiye Afisa Mkuu Mtendaji.

Kamau akiwa na Digrii ya Mawasiliano na Teknolojia (IT), naye Muchemi Stashahada ya Masuala ya Biashara, walitumia mtaji wa Sh500, 000 kuanza ufugaji-biashara wa nyuki.

Azma yao kufuga nyuki, pia ilichochewa na visa vya kuuziwa asali ambayo haikuwa na ubora unaofaa.

Walianza kwa kukodi kipande cha shamba Muhuri Road, karibu na Waiyaki Way, Nairobi.

“Hii ilikuwa baada ya kupata mafunzo kutoka kwa Taasisi ya Kitaifa Kuhusu Ufugaji Nyuki, ambayo ilitupevusha jinsi ya kufuga nyuki, kuwatunza na kuongeza thamani bidhaa zake,” Kamau anaelezea.

Miaka sita baadaye, wawili hao wanajivunia Waiyaki Way Beekeepers kutamba nchini.

Kamau, kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, alidokeza kwamba kando na masoko ya Nairobi na Kiambu, wametamba hadi Moyale, Eldoret, Busia, Kisumu, Mombasa, Nyeri, Meru, na Nakuru.

Kuanzia na shamba moja la kufuga nyuki, sasa wana matawi mengine katika Kaunti ya Kirinyaga na Naivasha.

“Tumeegemea sana kuongeza thamani bidhaa za nyuki, hususan asali,” Kamau anasema.

Bidhaa zingine wanazounda ni pamoja na mishumaa kwa kutumia nta (wax), sabuni, gundi ya nyuki, dawa ya nyuki kutibu vidonda, na mafuta.

Asali, Muchemi anasema huongezwa thamani ili kurefusha muda wa kudumu.

“Zipo taratatibu za kuchoma asali iliyovunwa – iliyoko kwenye nta kwa kutumia maji kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ili kuitenganisha,” Muchemi anafafanua.

Katika makao yao makuu Muhuri Road, wana kiwanda cha usindikaji asali, afisi na duka la kusambaza bidhaa zao.
Kilo moja ya asali iliyoongezwa thamani huuza Sh800.

Nairobi, wana mizinga jumla ya 20, Kirinyaga na Naivasha kila shamba likisitiri mizinga 25.

Kamau anasema mashamba yao huwapa kilo 300 kwa mwezi, na pia hupata kiwango sawa na hicho kutoka kwa wafugaji Narok na Baringo wenye kandarasi nao.

Mbali na urinaji asali na kuongeza thamani bidhaa za nyuki, Waiyaki Way Beekeepers pia hutoa huduma za mafunzo ya ufugaji wa viumbe hao wenye tija chungu nzima na uuzaji mizinga ya kisasa.

Kabla kuzamia ufugaji nyuki, hasa maeneo ya mijini, mkulima anapaswa kuwa na kibali kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).

Kando na faida zake za asali, nyuki husaidia katika uchavushaji.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *