Yabainika chanzo cha mzozo mpakani Narok-Kisii sio wizi wa mifugo pekee
IMEBAINIKA kuwa mgogoro unaoendelea katika mpaka wa Narok – Kisii eneo la Kiango unachochewa sio tu na wizi wa mifugo bali pia na mzozo wa mpaka na uchochezi kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.
Mgogoro huo ulianza zaidi ya wiki moja iliyopita katika eneo la Kiango baada ya madai ya wizi wa ng’ombe watatu, ambapo vijana waliokuwa na mishale, mapanga na silaha nyingine walishambuliana.
Inaripotiwa kuwa watu watatu wamefariki na wengine kadhaa kupata majeraha ya mishale. Mtu mmoja anayedaiwa kuwa mwizi wa mifugo sasa yuko mikononi mwa polisi.
Mnamo Jumatatu, Magavana Patrick Ole Ntutu (Narok) na Simba Arati (Kisii), viongozi wengine, wazee na wakazi kutoka jamii za Wamasai na Abagusii walikusanyika Kiango kwa mkutano wa amani.
Katika mkutano huo, madai yaliibuka kuwa vijana kutoka jamii moja wamepata mishale mipya n inayofanana wanayoitumia katika mapigano.
Madai haya yaliwasilishwa na Mbunge Obadiah Barongo wa Eneo Bunge la Bomachoge Borabu.
“Tunashangaa ni nani anayeweza kuwa anawapa mishale hawa vijana wanaopigana,” alisema Bw Barongo.
Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ole Ntutu, aliwakemea waliohudhuria mkutano huo wa amani, akidai kuwa walikuwa wepesi wa kuzungumza kuhusu amani lakini hawakueleza chanzo halisi cha tatizo.
‘Tafadhali, msituchezee akili mimi na Arati. Tatizo kati ya Wamasai na Wagusii ni nini? Hamlisemi, mnaongea tu kuhusu amani!’ alisema Gavana Ole Ntutu.
Aliendelea: ‘Mtafikiaje amani ikiwa hatubaini chanzo halisi cha tatizo hili?’
Kuhusu mgogoro wa mpaka, kuna mvutano kuhusu mipaka ya Mapashi-Nyamaiya katika shamba kubwa la Keyian.
Mnamo Jumatatu, wakazi waliripoti kuwa waliona vijikaratasi vilivyoelekeza sehemu ya jamii kurudi ilikotoka katika maeneo ya kaskazini mwa Bonde la Ufa.
“Lazima kuna watu wanaofadhili ghasia hizi kwa sababu wahalifu ni wachache tu, labda watatu au wanne. Lazima tukomeshe wahalifu hao,” alisema Gavana Arati.
Gavana Arati aliwasihi wazee na wanachama wa ‘Kamati ya Amani ya Mpaka’ kuhakikisha kuwa matukio ya wizi wa mifugo yanatatuliwa kwa njia ya amani.
“Nawaomba mhakikishe kwamba ng’ombe akipotea anatafutwa ipasavyo na kupatikana, ili kuepusha kuzuka kwa migogoro,” alisema.
Akizungumza katika mkutano tofauti Nairobi kuhusu mgogoro wa mpaka, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alikiri kuwa mzozo katika eneo la Trans Mara umeshughulikiwa vibaya, huku akiahidi kuwa serikali itarejesha hali ya kawaida.
Waziri Murkomen aliyasema haya katika mkutano na viongozi kutoka Kaunti za Kisii na Narok mjini Nairobi.
“Mapigano haya ni zaidi ya wizi wa ng’ombe. Yamegeuka kuwa chuki ya aina nyingine ambayo hatujawahi kushuhudia hivi karibuni. Hatutaruhusu uhalifu uendelee. Hatutaruhusu waendelee kuchoma mashamba ya miwa,” alisema Bw Murkomen.