Afueni diwani aliyetoweka miezi sita akipatikana

0

KIONGOZI wa Wachache kwenye Bunge la Kaunti ya Wajir Yussuf Ahmed Hussein ambaye alitoweka miezi sita iliyopita alisema alizuiliwa Nairobi kwa miezi miwili kisha kuhamishwa kusikojulikana.

Bw Hussein ambaye ni diwani wa wadi ya Dela alifika nyumbani kwake Mtaani Eastleigh saa tatu unusu Jumamosi usiku akiwa ameshikilia Quran mkononi.

“Alirudi nyumbani akiwa ameshikilia Quran. Mkewe alitupigia simu na tukathibitisha ni yeye,” akasema Elyas Abdille, binamuye diwani huyo.

Bw Abdille ambaye pia ni diwani wa wadi ya Dimtu, Kaunti ya Mandera, alisema familia hiyo ilimkimbiza Bw Hussein hadi hospitali ya Nairobi ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

“Alionekana yupo sawa japo kihisia alikuwa ameshtuka,” akasema Bw Abdille akimnukuu mkewe Bw Hussein.

Bado haikufahamika mahali ambapo diwani huyo alikuwa tangu atoweke Septemba 13, 2024 na jinsi alivyofika nyumbani. Ripoti ziliarifu alipelekwa Eastleigh, na watu wanaoaminika walimteka nyara.

“Alituambia alikuwa akizuiliwa na watu wengi Nairobi kwa miezi miwili kisha akahamishwa hadi eneo asikojua. Bado hatujajua nani alimwacha Eastleigh kwa sababu alikuja nyumbani pekee yake,” akasema Bw Abdille.

Mbunge wa Eldas Adan Keynan ambaye pia ni jamaa wa Bw Husseina kupitia chapisho kwenye X alithibitisha kurejea kwa diwani huyo.

“Alhamdulillahi,” Bw Keynan akaandika huku akifuatanisha na picha ya diwani huyo.

Bw Keynan  alikuwa kati ya viongozi wa Wajir na wakazi ambao walikusanyika nyumbani kwa diwani huyo Eastleigh kusherehekea kurejea kwake.

Gavana wa Wajir na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana  Nchini Ahmed Abdullahi alishukuru kuwa diwani huyo alirejea nyumbani akiwa hai.

“Alhamdulillahi. Nimefurahi Yussuf Hussein amepatikana na kuungana na familia yake baada ya miezi kadhaa. Tangu kutoweka kwake mnamo Septemba mwaka jana, watu wa Wajir wameumia na wamekuwa wakitia dua ili apatikane salama,” akaandika kwenye X.

Mbunge Mwakilishi wa Wajir Fatuma Abdi Jehow naye pia alimshukuru Mungu kwa kurejea kwa Bw Hussein salama.

“Sina maneno ila kusema Alhamdullilah kwa kurudi nyumbani kwa diwani wetu Yussuf,” akaandika kwenye ukurasa wake wa X.

Bw Hussein  alitoweka Nairobi mnamo Septemba 13, 2024 katika barabara ya Enterprise  akienda nyumbani kwake Pangani kutoka South C.

Ripoti zinaarifu kwa Bw Hussein alitekwa na watu waliokuwa na bunduki alipokuwa akiendeshwa kwenye teksi aliyokodisha. Watu hao waliziba teksi hiyo kisha wakamtoa na kumweka katika gari lao na kuenda naye.

Juhudi za wanafamilia na wanaharakati kumpata zilikosa kuzaa matunda kwa kuwa polisi walisema hawakujua mahali alikuwa. Mnamo Oktoba 2024, mwili uliondolewa Ziwa Yahud ambayo iliaminika ilikuwa ya diwani huyo.

Hata hivyo, uchunguzi wa sampuli ya DNA zilizochukuliwa zilionyesha kuwa mwili huo haukuwa wa diwani huyo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *