Amerika yaondoa raia wake Juba vita vikinukia
WASHINGTON, Amerika
WIZARA ya Masuala ya Kigeni ya Amerika imeamuru wafanyakazi wa ubalozi wake kuondoka jiji Juba Sudan Kusini huku taharuki ikitanda nchini humo baada ya mapigano yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo.
Agizo hilo lililotolewa Jumapili linaeleza kuwa mapigano hayo yameshika kasi “kwa sababu raia wanapata silaha kwa urahisi.”
Kundi moja la wapiganaji Jumanne lilipigana na jeshi la serikali na kupelekea kukamatwa kwa mawaziri wawili na naibu mkuu wa majeshi waaminifu kwa Makamu wa Rais wa Kwanza Riek Machar.
Boma la Dkt Machar lilizingirwa na wanajeshi huku wafuasi wake wakidai kukamatwa kwa maafisa hao watatu kutahujumu utekelezaji wa mkataba wa amani nchi Sudan Kusini.
Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia 2013 hadi 2018 wakati ambapo zaidi ya watu 4,000 waliuawa.
Rais Salva Kiir na Dkt Machar, aliyekuwa mpinzani wake, walitia saini mkataba wa amani mnamo 2018 ambao ungali unatekelezwa hadi wakati huu.
Mnamo Ijumaa, helikopta moja ya Amerika iliyokuwa ikiendesha shughuli ya uokoaji kaskazini mwa nchi hiyo ilishambuliwa .
Shirika moja la umoja wa mataifa la kutetea haki (UNCHR) lilitaja kitendo hicho kama “uhalifu wa kivita”.
Mnamo Jumamosi, shirika hilo lilielezea hofu kwa mapigani kaskazini mwa Sudan Kusini na taharuki jijini Juba, huenda “ikavuruga utekelezaji wa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini.”
“Tunashuhudia visa vya utovu wa usalama ambavyo vinaweza kurudisha nyuma hatua ambazo zimepigwa kuleta amani. Badala ya kuchochea migawanyiko na mapigano, sharti viongozi walenge kudumisha amani na kulinda haki za kibinadamu za raia wa Sudan Kusini huku wakikumbatia demokrasia,” akasema mwenyekiti wa shirika hilo Yasmin Sooka.