Bei ya sukari yafyatuka juu serikali ikianza sasa kutekeleza ada ya ustawishaji kilimo cha miwa
KUANZISHWA kwa Ada ya Ustawi wa Sekta ya Sukari (SDL) mnamo Februari 1, 2025, kumechangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo hadi Sh166.45 kwa kila kilo.
Bei hiyo ndiyo ya juu zaidi tangu Juni 2024 wakati ambapo kila kilo iliuzwa kwa Sh168.59, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.17 kutoka kwa Sh161. 34 mnamo Januari mwaka huu.
Ada hiyo inaweka ada ya asilimia nne kwenye sukari ambayo imezalishwa hapa nchini na ile ambayo inaingizwa nchini kutoka nje.
Ada hiyo inatumika kugharimia shughuli za Bodi ya Sukari Nchini (KSB), Taasisi ya Utafiti kuhusu Sukari, kudhibiti bei kwa wakuzaji wa miwa, kukarabati na kutengeneza viwanda na pia kuendeleza miundomsingi katika sekta ya sukari.
Viwanda vya sukari huwa vinatarajiwa kuwasilisha ada hiyo kwa KSB huku wale wanaoagiza sukari kutoka nje wakiwasilisha ada kwa KSB wenyewe au kupitia maajenti wao kufikia tarehe 10 ya kila mwezi.
Kutekelezwa kwa ada hiyo, kumekuja wakati ambapo pensheni inayokatwa na Hazina ya Kitaifa ya Kijamii (NSSF) pia imeongezwa huku waajiriwa wakiendelea kuumizwa na makato mengine katika utawala wa Kenya Kwanza.
Japo SDL inatarajiwa kuleta mageuzi yanayonufaisha sekta ya sukari, kupanda kwa bei ya kila kilo kutaumiza familia nyingi huku bei ya bidhaa nyingine pia zikiwa juu na gharama ya maisha kupanda.
Licha ya ongezeko hilo, bei ya sukari ipo chini kwa asilimia 16.78 ikilinganishwa na Sh200.1 kwa kila kilo mnamo Februari 2024.
Ongezeko la bei ya sukari mwaka jana, lilihusishwa au kushirikishwa na uhaba wa sukari duniani. India ilipiga marufuku ununuzi wa sukari kutoka Kenya na mataifa mengine.
Pia kupungua kwa sukari inayozalishwa nchini kwa sababu ya ukame kulichangia kupanda kwa bei yake.
Hali hiyo ilisababisha serikali kuondoa ushuru kwenye sukari ambayo inaingizwa nchini. Hata hivyo, uagizaji huo uliongeza sukari sokoni ikizingatiwa uzalishaji pia ulipanda baadaye na kudhibiti bei ya sukari sokoni.
Uagizaji kutoka nje ulipungua kutoka tani 162,189.1 kwenye robo ya tatu mnamo 2023 hadi tani 88,372 muda sawa na huo mnamo 2024 na kufanya bei kuwa dhabiti.
Utawala wa Rais William Ruto umekuwa mstari wa mbele katika kufufua sekta ya sukari ambayo ilikuwa ikielekea kuangamia ili wakulima wa miwa nao wanufaike.
Kutiwa saini kwa Sheria ya Sukari 2024, kunalenga kuhakikisha changamoto ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi zinatatuliwa. Kati ya changamoto hizo ni kupungua kwa uzalishaji, ushindani kwa sukari ya Kenya na ile inayotoka nje pamoja na sera zilizopitwa na wakati.