Chepkirui azoa Sh32 milioni Nagoya Marathon
SHEILA Chepkirui aliweka Kenya kwenye ramani ya dunia baada ya kubeba taji la mbio za wanawake pekee za Nagoya Marathon nchini Japan, Jumapili.
Chepkirui, 34, ambaye alishinda New York Marathon nchini Amerika mwaka jana, aliwatoka wapinzani wake wa karibu Sayaka Sato (Japan) na Eunice Chumba (Bahrain) zikisalia kilomita sita na kukata utepe wa mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:20:40.
Sato aliridhika na nafasi ya pili kwa 2:20:59 naye mshindi wa Michezo ya Bara Asia mwaka 2023 Chumba akafunga tatu-bora kwa 2:21:35.
Chepkirui na Chumba walikuwa mbele kufikia kilomita ya 33 wakiwaacha Sato na Mjapani mwenzake Rika Kaseda. Hata hivyo, Sato alitoka nyuma na kumpita Chumba zikisalia kilomita sita na kuimarisha muda wake bora kwa zaidi ya dakika moja.
“Nafurahia sana ushindi huu. Nashukuru Mungu kwa kunipa afya nzuri na nguvu ambazo zimeniwezesha kukamata nambari moja. Napata nguvu kutoka kwa kufanya mazoezi na pia kuwa na mtazamo mzuri”
Chepkirui alizoa tuzo ya Sh32 milioni (Dola za Amerika 250,000) kwa ushindi huo.

Nchini Ureno, Wakenya Ruth Chepngetich na Shadrack Kipkemei waliridhika na nafasi ya pili katika mbio za Lisbon Half Marathon. Tsigie Gebreselama aliibuka malkia kwa kukamilisha 21km kwa saa 1:04:21 akifuatiwa na Chepngetich (1:06:20) na Mswidi Abeba Aregawi (1:06:36).
Kipkemei (dakika 59:49) alimaliza katikati ya Abdi Waiss (59:44) na Mohamed Ismail (59:54) kutoka Djibouti. Kuvunja rekodi ya dunia ya 21km kwenye Lisbon Half kunaandamana na bonasi ya Sh14 milioni.
Nchini Ufaransa, Kennedy Kimutai (1:00:16), Timothy Kosgei (1:00:22) na Timothy Kibet (1:00:44) walifagia nafasi tatu za kwanza za wanaume za Paris Half Marathon nao Jackline Cherono (1:07:16) na Christine Kioko (1:09:55) wakawa nambari moja na tatu kwa upande wa kinadada.
Muethiopia Muluhabt Tsega (1:08:34) alimaliza nyuma ya Cherono.Erick Sang naye alitawazwa mshindi wa Loop Den Haag Half Marathon kwa dakika 59:38 akifuatwa na Filex Kibet (saa 1:00:50) na Peter Tuitoek (1:01:03) nchini Uholanzi.
Emily Chebet aliridhika na nafasi ya tatu kwa upande wa wanawake kwa 1:09:47, nyuma ya Muethiopia Mikedes Shimeles (1:08:17) na Mjerumani Gesa Krause (1:09:46).