Daraja hatari Ololulunga lililopindika na kutingika wakazi wanapopita
DARAJA la Oleshapani – Ololoipangi katika wadi ya Ololulunga eneo bunge la Narok Kusini linatatiza huduma za usafiri kutokana na ujenzi mbovu ambao unasababisha kutingika wakati wapitanjia na waendesha magari wanapotumia.
Daraja hilo ambalo lilijengwa mwaka wa 2007 na aliyekuwa Mbunge Lankas Ole Nkoidila ili kurahisisha huduma za usafiri, kwa sasa linahatarisha maisha na kusababisha ajali kufuatia magari na mifugo kuanguka kwenye mto.
Daraja hilo la kuogofya limewalazimisha wahudumu wa bodaboda na wanaotumia magari kupita kwenye mto ambao pia ni hatari, haswa wakati wa mafuriko.
Mkazi Bw Robert Korir anasema hali hiyo inafanya baadhi ya wakazi kushindwa kulipa karo ya wana wao kufuatia mazao yao ya viazi, mboga mahindi na vitunguu kuharibika kabla ya kufika katika soko kuu.
“Hizo bidhaa ukiangalia ni vitu ambavyo vinatupa pesa nyingi lakini sasa shida kabla ufikishe hayo mazao kwa lami, utakuwa umeteseka sana. Heri hizi pesa zikae na watutengenezee barabara tuwe tunajitafutia vitu vyetu kuliko tukae hivyo,” alisema Bw Korir.
“Saa hii nina wanafunzi wawili ambao nimeshindwa kulipia karo yao. Tunaomba hawa viongozi wetu watusaidie ili tujisaidie wenyewe.”
Daraja hilo la Oleshapani – Ololoipangi ambalo linatingika, limemlazimisha mhudumu wa Bodaboda Bw Amos Langat kupitia ndani ya mto kuepuka kuanguka ndani.
Aliwaomba viongozi wa eneo hilo kupatia ujenzi wa daraja hilo kipao mbele na kuacha kushughulikia miradi ya stima na kuweka barabara ya lami.

“Tunafika upande ule mwingine tukiwa maji tupu. Tunakaa nikama tulikuwa tunachezea kwenye matope. Wiki jana Machi 7, 2025 gari la Probox lilipoteza mwelekeo wake na kutumbukia mtoni. Likiwa limebeba abiria wanne ambao waliumia. Walio na magari kutoka eneo hili wameacha magari yao nyumbani kwa kuhofia kuanguka,” aliesema Bw Langat.
Mwanaharakati wa vijana katika wadi hiyo Bw Sarisar Bett, 38, alitaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuzuia matukio zaidi na kuhakikisha usalama wa wote wanaotumia daraja hilo linalosikitisha. Aliwataka viongozi hao kuepuka mabroka ambao wamechangia kujikokota kwa huduma hizo kutekelezwa.
“Kama kaunti, tumekuwa mstari wa mbele kuongoza kwenye mapato. Maendeleo hayaambatani na ushuru uliokusanywa na kaunti. Sisi raia tumeteseka sana.”
Mbunge wa eneo hilo Bw Kitilai Ole Ntutu alisema daraja hilo muhimu hutumiwa na zaidi ya wakazi 2000 kila siku, akidai hakuna rekodi za awali zilizoonyesha ujenzi awali ulitumia fedha ngapi.
Hata hivyo alisema ujenzi wa daraja hilo umekabidhiwa mamlaka ya barabara za vijijini nchini (KeRRA) baada ya kufanya mkutano na mkurugenzi wa mamlaka hiyo majuma mawili yaliyopita.
“Wiki iliyopita KeRRA ilituma maafisa wake kwa ushirikiano na Wanajeshi wa nchi kufanya vipimo. Wahandisi anafanya hesabu zake kujua ujenzi wa daraja lipya utagharimu pesa ngapi.”