Kioja jijini Nairobi, mwanamume akijaribu kujiua kwa kujiteketeza nje ya Mahakama ya Juu

0

IDARA ya Mahakama inachunguza kiini cha hatua ya mwanamume mmoja kujiteketeza nje ya majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi Jumanne, Machi 11, 2025.

Kwenye taarifa aliyotoa baada ya mwanamume huyo kuokolewa na maafisa wa polisi na kukimbizwa hospitalini, msemaji wa idara hiyo Paul Ndemo alisema wanachunguza kubaini ikiwa kisa hicho kinahusiana na kesi iliyoko mahakamani.

“Tunataraji kuwa baada ya mwanamume huyo kutibiwa, polisi watamhoji kubaini chanzo cha kitendo chake cha kiajabu. Idara ya Mahakama inafuatilia kwa makini suala hilo kwa lengo ya kutaka kujua ikiwa hatua ya mtu huyo kutaka kujitoa uhai inaweza kuhusiana na suala lililoko mahakamani,” Bw Ndemo akasema.

“Tunamtakia afueni ya haraka,” afisa huyo akaongeza.

Kwenye taarifa yake, Bw Ndemo alisema mwanamume huyo ambaye hakutambuliwa, akitembea katika barabara ya City Hall Way, alisimama nje ya majengo ya Mahakama ya Juu.

“Alikuwa amebeba stakabadhi fulani na chupa yenye kitu fulani majimaji. Akiwa amesimama kwenye veranda aliweka stakabadhi hizo chini, akajimwagia maji hayo yaliyoaminika kuwa petroli akatoa kiberiti na kujiwasha moto,” Bw Ndemo akaeleza.

Kulingana na msemaji huyo wa Idara ya Mahakama, maafisa wa usalama katika Majengo ya Mahakama ya Juu walifika hapo haraka na kumwokoa mwanamue huyo kwa kuuzima moto huo.

Bw Ndemo alisema mwanamume huyo alipata majeraha mabaya baada ya stakabadhi hizo na nguo zake kuteketea.

Alieleza kuwa maafisa hao walisaka usaidizi kutoka kwa maafisa wa polisi walioko katika Kituo cha Polisi cha jumba la KICC.

“Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilipashwa habari na ikatoa ambulansi. Maafisa wa polisi walimweka mwanamume huyo ndani ya ambulansi hiyo na wakamkimbiza hadi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” akasema Bw Ndemo.

Baadhi ya Wakenya wanaosaka haki katika mahakama za humu nchini wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa uamuzi kuhusu kesi zao na hivyo kuhisi kinyumwa haki.

Baadhi ya kesi, haswa zinazohusu mzozo wa ardhi, hujivuta mahakama kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kuamuliwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *