MAONI: McCarthy akipewa sapoti ya kutosha, Harambee Stars itakuwa moto wa kuotea mbali
KOCHA mpya wa Harambee Stars Benni McCarthy akipewa sapoti ya kutosha kutoka kwa serikali, Shirikisho la Soka nchini (FKF) pamoja na wafuasi wa soka nchini, ataleta mabadiliko makubwa katika timu ya taifa kutokana na tajriba yake.
Jumatatu, kocha huyo wa zamani wa Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alitangwaza rasmi kama kocha mkuu kuchukua nafasi ya kocha wa muda Francis Kimanzi kwa mkataba wa miaka miwili.
Kimanzi alitwikwa majukumu hayo Desemba mwaka jana baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Engin Firat kujiuzulu kutokana na kutolipwa mishahara.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini ya almaarufu “Bafana Bafana”, ana kibarua kigumu mwezi huu kuongoza Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwakani dhidi ya Gambia ugenini mnamo Machi 24 na Gabon nyumbani siku nne baadaye.
Kenya ipo Kundi F na alama tano katika nafasi ya nne pamoja na Ivory Coast wanaoongoza kundi na alama 10, Gabon nafasi ya pili na alama tisa na Burundi wakiwa nafasi ya tatu na alama saba.
Gambia (alama tatu) na Ushelisheli (bila alama) wakiwa nafasi ya tano na sita mtawalia.
Baada ya michuano hiyo, ataanza kuandaa timu ya Stars kwa Michuano ya Afrika (CHAN) ambayo inahusisha wachezaji ambao wanacheza ligi ya ndani mwezi Agosti.
Mtego mwingine utakuwa kuionoa Stars kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambapo Kenya ilifuzu moja kwa moja.
Mashindano yote mawili yataandaliwa kwa ushirikiano na Kenya, Uganda na Tanzania.
Huu sasa utakuwa ni mtego mkubwa kwake kuona ikiwa anaweza kazi hii na natumai ameelezwa kwamba, Wakenya wakati mwingine hawana subra linapotekea suala la timu za taifa za soka.
Isitoshe, kulikuwa na hisia mseto kutoka kwa wachezaji wa zamani wa Stars wakati kulitokea fununu kwamba, McCarthy atakuwa kocha miezi sita iliyopita.
Wengi walihisi walistahili kupewa majukumu hayo huku wengine wakikumbatia ujio wake.