MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tuhusishe uhusiano wetu na Kurani katika mfungo
SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na nyingine ndogondogo, swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu ‘Alayhi wasallam, maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi siku ya Kiyama.
Hakika mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur’an, kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu katika Qur’an Tukufu:
“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za wongofu na upambanuzi.” (Al-Baqarah: 185).
Mwezi huu ni wakati wa kuhuisha uhusiano wetu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kusoma, kujifunza, na kutafakari maana zake.
Kusoma Qur’an katika mwezi wa Ramadhani kuna malipo makubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hadithi ya Ibn ‘Abbas inatufahamisha kuwa Jibril alikuwa akikutana na Mtume Muhammad (Swallallahu ‘Alayhi wasallam) kila usiku wa Ramadhani ili kumsomesha Qur’an.
Hii inaonyesha kuwa Qur’an ina nafasi ya pekee katika mwezi huu, na waumini wanapaswa kuiga Sunnah hii kwa kuzidisha usomaji na kuzingatia mafundisho yake.
Qur’an ni nuru na mwongozo kwa waumini, na mwenye kuisoma hujipatia baraka kubwa. Katika hadithi nyingine, Mtume (Swallallahu ‘Alayhi wasallam) amesema: “Anayesoma herufi moja kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu atapata thawabu kumi.” (Tirmidhi).
Je, ni vipi thawabu hizi zinavyoongezeka katika mwezi wa Ramadhani, ambao kila tendo jema huzidishiwa malipo mara nyingi zaidi?
Pamoja na kusoma, ni muhimu pia kujitahidi kuelewa maana na kutekeleza maagizo ya Qur’an katika maisha yetu. Mwezi huu ni fursa ya kujisafisha, kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa toba, na kuimarisha ibada. Tuige mfano wa Salafus Swalih, waliokuwa wakikamilisha khitma nyingi za Qur’an katika mwezi huu mtukufu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atufanye miongoni mwa wanaoshughulika na Qur’an, kuisoma, kuizingatia, na kuifuata. Atujaalie Ramadhani hii iwe yenye baraka kwetu na atuandikie kuwa miongoni mwa waliokombolewa na Moto wa Jahannam. Ameen.