Miradi hatarini kaunti zikikosa kutumia Sh72b
MIRADI ya kaunti kuhusu afya, elimu na barabara inakabiliwa na hatari kubwa ya kukwama baada ya serikali za kaunti kukosa kutumia Sh72 bilioni za bajeti ya maendeleo katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2024.
Kulingana na ripoti ya hivi punde ya mdhibiti wa bajeti (COB), Serikali za kaunti zilitumia Sh33.6 bilioni – ambazo ni thuluthi moja tu ya Sh105.7 bilioni ambazo zilihitajika kutumiwa katika maendeleo.
Katika mwaka wa kifedha kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025, kaunti zina bajeti ya maendeleo ya Sh211.5 bilioni. Kushindwa kutumia Sh72 bilioni kwa miradi ya maendeleo kulisababishwa na mapato duni yaliyokusanywa na kila kaunti (OSR) na ucheleweshaji wa mgao kutoka Serikali ya Kitaifa.
“Uchambuzi wa matumizi ya pesa za maendeleo kama sehemu ya bajeti ya maendeleo ya kila mwaka iliyoidhinishwa ulionyesha kuwa serikali kadhaa za kaunti zilikuwa na kiwango cha utumiaji wa chini ya asilimia 10 kwa mipango yao ya maendeleo,” COB, Dkt Margaret Nyakang’o alifichua.
Kaunti hizo sasa zimesalia na kibarua cha kutumia zaidi ya Sh177.9 bilioni kwa miradi ndani ya miezi sita inayokamilika Juni 2025, jambo ambalo linazua hofu ya kukwama kwa miradi na ongezeko la madeni ambayo hazijalipa.
Sheria inataka angalau asilimia 30 ya bajeti za kaunti zitengewe maendeleo lakini serikali za kaunti zimekuwa zikikiuka hitaji hilo kwa miaka mingi, jambo ambalo COB sasa anasema inatia wasiwasi.
“Mipango thabiti ya upangaji, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi inapaswa kupitishwa ili kuboresha kiwango cha matumizi ya fedha za maendeleo na kuimarisha maendeleo ya nchi,” Dkt Nyakang’o anasema.
Matumizi ya maendeleo katika kipindi hicho, hata hivyo, yaliongezeka kutoka Sh24.8 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka wa 2023.
Ripoti ya COB inabainisha kuwa katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2024, Kaunti ya Mandera ilikuwa na matumizi ya juu zaidi ya maendeleo dhidi ya bajeti yake ya maendeleo ya kila mwaka kwa asilimia 32.Kaunti ya Narok ilitumia Sh1.5 bilioni (asilimia 30 ya bajeti yake ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka huo), Kaunti ya Garissa ilitumia Sh1.18 bilioni (asilimia 28), Kaunti ya Uasin Gishu ilitumia Sh1.28 bilioni (asilimia 27) na Marsabit ilitumia Sh974 milioni (asilimia 26).
“Kinyume chake, Kaunti zifuatazo zilifikia viwango vya chini zaidi vya utumiaji wa bajeti zao za maendeleo zilizoidhinishwa;Baringo na Tana River kwa asilimia 7, na Taita-Taveta, Kisumu, Nairobi City na Nyeri kwa asilimia 6 na Elgeyo-Marakwet, Lamu, Nakuru na Kitui kila moja kwa asilimia 5,” ripoti ya COB inabainisha.