Polisi wamiminia risasi washukiwa wa ujambazi waliokuwa wanatoroka kwa Tuktuk

0

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Kisii wamewaua kwa kuwapiga risasi washukiwa wanne wa ujambazi.

Polisi hao pia wamewanasa washukiwa wengine wawili wa uhalifu katika matukio mawili tofauti yaliyofanyika usiku wa kuamkia Alhamisi.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii Charles Kases, katika kisa cha kwanza, walipokea taarifa kutoka kwa umma kuhusu watu waliokuwa wakivunja maduka ya watu katika mji wa Marani.

Baada ya taarifa hizo kutolewa, polisi hao walikimbia kwenda kuwakabili na walipofika, walikuta washukiwa hao wameondoka na wakaanza kuwaandama.

“Maafisa wetu waliwafuata kwenda eneo la Sombogo na walipowakaribia, washukiwa hao walianza kuwafyatulia maafisa wetu risasi. Makabiliano baina ya pande hizo mbili yalijiri na kwa bahati mbaya, washukiwa hao walipata majeraha mabaya ya risasi yaliyokatiza maisha yao,” Kamanda Kases alisema.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii Charles Kases (kulia) akizungumza na wanahabari kuhusu uhalifu Kisii. Picha|Wycliffe Nyaberi

Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa bado watu hawo hawajajulikana. Aliongeza kuwa walikuwa wakitoroka kutumia tuktuk.

Katika kisa cha pili, polisi waliwakamata washukiwa wengine wawili wa ujambazi katika kituo cha petroli cha Texas, kilichoko mjini Kisii.

Kulingana na polisi, wawili hao ni baadhi ya genge ambalo limekuwa likiwahangaisha wakazi katika mji wa Suneka kwa wizi wa kimabavu.

Wawili hao walitambuliwa kama James Ochieng na Gerald Okumu, waliokuwa wakisafiria pikipiki. Baada ya kufanyiwa msako, walipatikana na bastola ndogo na risasi tano. Pia walipatikana na vyuma vya kubuni ambavyo kulingana na kamanda Kases vinaweza kufyatua risasi.

Wawili hao walifikishwa mahakamani ambapo polisi waliomba wapewe kibali cha kuwazuia kwa siku 30 ili kukamilisha uchunguzi wao.

Kamanda Kases aliwahakikishia wakazi wa Kisii hasa wafanyabiashara kuwa watafanya kila wawezalo ili kuwalinda dhidi ya uhalifu wowote.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *