Raila afichua alikataa kutia saini mkataba uliotayarishwa akiwa nje ya nchi

0

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga jana alifichua kwamba alikataa kutia saini mkataba na Rais William Ruto walipokutana Mombasa baada yake kurejea nchini wiki moja baada ya kushindwa katika uchaguzi wa uenyekiti wa Muungano wa Afrika.

Baada ya uchaguzi huo uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, Raila alielekea Dubai kwa wiki moja kupumzika na aliporejea alielekea moja kwa moja hadi Mombasa ambako alikutana na Rais Ruto aliyekuwa katika ziara ya kikazi pwani.

Viongozi hao walitumia fursa hiyo kueleza kuwa wangeendelea kushirikiana katika siasa za humu nchini.

Wandani wa Rais Ruto walipendekeza ateuliwe wadhifa serikalini ili nchi inufaike na uzoefu wake wa miaka mingi.

Bw Odinga alitangaza kuwa angeshauriana na wafuasi wake kote nchini kabla ya kutangaza mwelekeo wa kisiasa wakati ambao viongozi wa upinzani walikuwa wakimrai ajiunge nao.

Jana, Bw Odinga alisema chama chake cha ODM na kile cha UDA cha Rais Ruto vilikuwa vimetayarisha makubaliano ya ushirikiano lakini hakutia saini ili ashauriane na wafuasi wake.

“Niliporudi, nilikutana na Rais Mombasa akaniambia nisaini hati, lakini ilinibidi kushauriana, nilienda kaunti mbalimbali kutafuta maoni, na sasa tuko hapa,” Bw Odinga alisema jana baada ya kutia rasmi mkataba wa ushirikiano na serikali.

“Lengo la sasa la MOU ni kusaidia kupunguza mivutano iliyopo nchini, kusaidia watu, kupunguza mateso yao, na kupeleka nchi mbele kwa kushughulikia changamoto muhimu za kijamii, kisiasa na kiuchumi,” Bw Odinga alisema.

Katika MOU hii, tunakubali kuanza hatua za kurekebisha vipaumbele vya nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kushughulikia ajenda ya vijana ambayo imepuuzwa katika miaka 62 iliyopita ya uhuru wetu.

Kwa upande wake Rais Ruto alifichua kwamba baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 ambao Raila alikuwa mpinzani wake mkuu, alimpigia simu waziri mkuu huyo wa zamani kumhakikishia anavyomheshimu.

“ Nilimwambia nitaishi kumheshimu. Ni watu wachache sana wanaweza kutanguliza maslahi ya taifa na wananchi mbele ya maslahi yao binafsi. Ndugu yangu Raila, historia itakuhukumu kwa haki kwa ulichoifanyia nchi hii,’ alisema Rais Ruto ambaye alianza kwa kukumbusha hadhira kwamba alikuwa mmoja wa waanzilishi wa ODM na Raila alikuwa kiongozi wake chamani.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *