Raila, bingwa wa ujanja wa kisiasa
RAILA Odinga amejipata tena katika nafasi ya mamlaka na ushawishi ndani ya serikali ya Rais William Ruto, akithibitisha tena umahiri wake kama mwanasiasa anayeweza kustahimili dhoruba za kisiasa nchini.
Bw Odinga, kupitia chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM), Ijumaa alitia rasmi makubaliano ya kisiasa na Rais Ruto, akifanya hii kuwa mara yake ya nne ya kufanya ‘muafaka wa kisiasa’ na serikali na wapinzani wake katika uchaguzi.
Kwa Bw Odinga, makubaliano yake na walioko serikalini yalianza mwaka wa 1998 alipoingia katika ushirikiano wa kisiasa na Rais Daniel Moi, ambao baadaye uligeuka kuwa muungano kati ya chama chake cha National Democratic Party (NDP) na KANU mnamo 2002. Kisha aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Katibu Mkuu wa KANU. Mwaka wa 2008, alitia saini mkataba wa Serikali ya Muungano uliofanikishwa na Kofi Annan na Rais Mwai Kibaki, jambo lililomfanya kuwa Waziri Mkuu na kumaliza machafuko ya baada ya uchaguzi.
Baada ya kushindwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2013, Bw Odinga alianza harakati za ukusanyaji saini kwa ajili ya kura ya maamuzi ya Okoa Kenya, ambayo mwaka wa 2016 ilikataliwa na tume ya uchaguzi kwa msingi kwamba ni saini 891,598 pekee kati ya milioni 1.6 zilizowasilishwa na muungano wa Cord zilizothibitishwa kuwa halali.
Baadaye alitumia juhudi hizo kushinikiza kuondolewa kwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Issack Hassan, na makamishna wake, jambo lililotokea mwishoni mwa 2016. Tume mpya iliyoongozwa na Wafula Chebukati, ambaye alifariki mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 63, iliapishwa Januari 2017 na kumaliza muhula wake Januari 2023.
Baada ya uchaguzi wa 2017, ambapo Rais Kenyatta alitangazwa mshindi lakini matokeo yakabatilishwa na Mahakama ya Juu, Bw Odinga alisusia marudio ya uchaguzi mnamo Oktoba na kuongoza maandamano yaliyoshinikiza kuondolewa kwa serikali na IEBC.
Kisha alifanya mwafaka na Rais Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, maarufu kama “handisheki”, kumaliza miezi ya maandamano ya ghasia na kuingia katika kile ambacho makamu wa rais wa wakati huo, William Ruto, baadaye alikiita “mfumo wa utawala usioeleweka, ambapo haikujulikani ikiwa ni upinzani ndani ya serikali au serikali ndani ya upinzani.”
Japo awali aliapa kutokubali mpango wowote wa kushirikiana na serikali, mnamo 2023 alilegeza kamba na kuitisha kuundwa kwa Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco), ambayo ilijadili masuala na kupendekeza, miongoni mwa mambo mengine, kuanzishwa kwa afisi ya Waziri Mkuu na Kiongozi Rasmi wa Upinzani.
Hata hivyo, ucheleweshaji wa utekelezaji wa mapendekezo hayo bungeni na maandamano ya vijana dhidi ya ushuru mkubwa na utawala mbaya mnamo Juni 2024 yalirejesha mazungumzo haya, na kusababisha kujumuishwa kwa washirika muhimu wa Bw Odinga ndani ya serikali.Lakini hilo halikutosha.
Rais Ruto kisha alimpigia debe Bw Odinga kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), nafasi ambayo alipoteza mnamo Februari mwaka huu.
Akiwa anakabiliwa na upinzani unaokua kutoka kwa aliyekuwa naibu wake aliyeondolewa mamlakani, Rigathi Gachagua, makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, na kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua miongoni mwa wengine, Dkt Ruto alichukua hatua kali: Alitia saini mkataba wa ushirikiano kati ya chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na ODM cha Bw Odinga.
Na kwa hatua hiyo, Bw Odinga ameinuka tena kuwa na ushawishi ndani ya serikali ya Kenya Kwanza, ambayo viongozi wake – wakati wa uchaguzi wa 2022 – waliwataka wapiga kura kumpeleka nyumbani kwake Bondo akastaafu siasa.
“Tunaweka wazi kuwa makubaliano tuliyotia saini leo hayamaanishi kuundwa kwa muungano wa kisiasa kati ya ODM na UDA. Hata hivyo, utekelezaji wake kwa mafanikio unaweza kuwa msingi wa hatua za kuelekea kuanzishwa kwa taifa lenye utulivu katika siku zijazo,” alieleza Bw Odinga siku ya Ijumaa wakati wa kutia saini makubaliano hayo.
Lakini washirika wa Waziri Mkuu wa zamani tayari wanashikilia nyadhifa za uwaziri serikalini na bungeni.
Katika Bunge, Rais Ruto anaowaondoa washirika wa Rigathi Gachagua ili kutoa nafasi kwa washirika wa Bw Odinga.
Katika Baraza la Mawaziri, Dkt Ruto amemjumuisha John Mbadi (Hazina ya Kitaifa), Opiyo Wandayi (Nishati na Petroli), Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Majini), Wycliffe Oparanya (Ushirika) na Beatrice Askul (Jumuiya ya Afrika Mashariki na ASAL).
Ushirikiano huu wa kisiasa si tofauti na makubaliano mengine ya kisiasa ambayo Bw Odinga amekuwa nayo na marais wa zamani, ambao mara ya kwanza alikuwa amepambana nao katika uchaguzi kabla ya kufanya mwafaka nao.
Katika hali nyingi, Bw Odinga amekuwa mnufaika mkubwa, akijiboresha kwa vita vya kisiasa vijavyo na kupata nafasi za ushawishi kwa ajili yake na washirika wake.
“Umoja huu mliounda leo si kwa ajili yenu wawili pekee, kwa sababu Baba ameona yote; kwa hakika, ana vya kutosha kwa vizazi vyote. Rais ameshikilia nyadhifa zote. Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu, umoja huu ni kwa ajili ya vijana, wanawake, makundi yaliyotengwa..ni kwa Wakenya wote ambao wamehisi kama hawajawahi kuwa sehemu ya Kenya,” alisema Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, Gladys Wanga, ambaye pia ni Gavana wa Homa Bay.
Bw Odinga kwa mara ya kwanza alifanya muungano wa kisiasa na Rais mstaafu Daniel Moi mnamo 1998 baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1997, ambapo Bw Odinga, aliyekuwa wa tatu baada ya Moi na Mwai Kibaki, kukutana na Rais Moi katika makazi yake ya Kabarak, Nakuru na kukubaliana kushirikiana kati ya KANU na chama chake cha National Development Party (NDP).
Kisha mnamo 2001, Bw Odinga alihalalisha ushirikiano huu kwa muungano kati ya NDP na chama tawala cha KANU wakati huo. Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ‘New KANU’.

Bw Odinga alifanya uamuzi huo baada ya kumenyana na Moi katika uchaguzi wa 1997, ambapo aligombea urais kwa mara ya kwanza.
Katika makubaliano hayo, Bw Odinga aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa KANU, huku Rais Moi akimpa wadhifa wa Waziri wa Nishati.
Prof David Monda, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Amerika na mchambuzi wa siasa, anasema kuwa Bw Odinga ni “mwanasiasa aliyebobea katika kujiokoa kisiasa na ambaye mara zote huweka maslahi yake ya kisiasa mbele.”
“Tabia hii inaathiri mbinu zake katika siasa za kitaifa, iwe ni ushirikiano wake na Moi kupitia NDP, mwafaka na Kibaki na Uhuru, au maridhiano yanayoendelea na Ruto,” anasema Prof Monda.
Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, anasema kuwa siasa ni mchezo wa kubadilishana maslahi na kufanya maelewano.
“Swali la msingi basi ni iwapo maslahi hayo na maelewano yanayofanywa yanasaidia siasa za maendeleo kwa manufaa ya wengi au yanahudumia tu maslahi finyu ya kisiasa au binafsi?” aliuliza Bw Omondi.
Mnamo 2007 – baada ya ghasia za baada ya uchaguzi zilizosababishwa na matokeo tata ya urais – Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Kenya chini ya serikali ya Muungano Mkuu iliyopatanishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan.
“Mwafaka mara nyingi humpa mtaji wa kisiasa unaohitajika ili kuleta utulivu na amani. Anaweza asiwe mwokozi wa mwisho wa siasa za Kenya, lakini ni mtaalamu wa mazungumzo ya kisiasa ambaye hajawahi kuingia katika mazungumzo bila kuwa na mkakati. Ni kisu chake cha kisiasa kinachomwezesha kujikatia sehemu kubwa kwa maslahi yake,” anasema mchambuzi wa siasa, Bw Javas Bigambo.
Prof Monda anasema kuwa baadhi ya mbinu hizi za kisiasa ni za muda mfupi, za kuepuka matatizo, na za kimikakati.