Serikali: La, hatujauzia Mturuki Bomas Of Kenya inavyodaiwa, tunafanya tu ukarabati

0

SERIKALI Jumatatu ilikanusha vikali madai ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuwa kuna mpango wa kuuza Bomas of Kenya kwa raia wa Uturuki.

Katibu katika Idara ya Utamaduni na Turathi Ummi Mohamed Bashir jana alisema kauli ya Bw Gachagua ilikuwa ni uongo ambao unastahili kupuuzwa na Wakenya.

Kupitia taarifa, katibu huyo alisema Bw Gachagua alikuwa kwenye baraza la mawaziri ambalo liliidhinisha kukarabatiwa kwa Bomas of Kenya ili ifike hadhi ya kimataifa na inashangaza sasa anaeneza porojo kuhusu suala hilo.

“Kustawishwa kwa Bomas kuliidhinishwa na Baraza la Mawaziri mnamo Agosti 8, 2023  baada ya ombi hilo kuwasilishwa na aliyekuwa waziri wa utalii Peninah Malonza,” akasema Bi Mohamed.

“Hii ina maana kuwa Bw Gachagua alikuwa kwenye baraza la mawaziri suala hilo likipitishwa kwa kuwa alitimuliwa uongozini mnamo Oktoba 2024.”

Alishikilia kuwa Bomas haijauzwa na kuwa mpango wa kuikarabati umekwepo kwa miaka 10 iliyopita hata wakati serikali za awali zilikuwa mamlakani.

“Bomas haijauzwa na wazo la kuikarabati limekwepo kwa miaka 10. Ni utawala huu ndio umechukulia suala hilo kwa uzito na kuanza kulitekeleza,” akaongeza.

Katibu huyo alisema kuwa Bomas ina cheti cha umiliki ardhi ambacho kilitolewa mnamo 1991 na kimehifadhiwa na serikali.

Alisema ukarabati huo utapandisha hadhi ya Bomas ili ifike kiwango cha kimataifa na kiwe na ukumbi wa kisasa wa kuandaa mikutano ya kimataifa.

“Bomas itakuwa ikijiuza pekee kama kitovu cha kitalii na mikutano na itakuwa hatua zaidi mbele kuliko hali ya sasa ambayo imekwepo kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita,” akasema Bi Mohamed.

Akihudhuria ibada ya kanisa Kaunti ya Kajiado, Bw Gachagua alidai kuwa ndiye pekee kwenye baraza la mawaziri ambaye alipinga pendekezo aliloladai lilitolewa kuuza Bomas of Kenya.

“Bomas imeenda kwa sababu mauzo yake yaliletwa kwenye baraza la mawaziri nami nikapinga. Mawaziri wengine waliogopa kwa sababu wakimwona rais wanaanza kutetemeka,” akasema Bw Gachagua.

“Ni mimi pekee nilisimama na kusema Bomas of Kenya ni turathi ya kitaifa na haiwezi kuuzwa,” akaongeza.

Bw Gachagua alisema Wakenya wako kivyao kwa sababu Rais Ruto sasa anaweza kufanya chochote ikiwemo kuuza Bomas of Kenya kwa sababu hakuna mwenye ujasiri wa kumpinga serikalini.

“Ni Mungu tu atatusaidia kwa sababu hao wengine wanafuata tu mkondo,” akasema naibu huyo wa rais wa zamani.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *