TAHARIRI: Raila ana fursa ya kumshawishi Ruto aimarike
BAADA ya juhudi kadhaa za kumrai Rais William Ruto abadili baadhi ya mipango yake kukosa kufaulu, sasa Rais ana nafasi moja ya kuokoa hatima yake.
Miongoni mwa mipango inayotishia kufaulu kwa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao, ni Ushuru wa Nyumba. Pia Bima mpya ya Afya ya Jamii (SHA) ina kasoro.
Kadhalika, mfumo wa ufadhili wa elimu ya vyuo vya kadri na vyuo vikuu unaonekana kushindwa kufanya kazi huku ukabila katika ajira ukionekana kukolea hasa katika awamu ya kwanza ya utawala wa Kenya Kwanza.
Jambo la kwanza kabisa ni kujaribu kumwelewesha Rais Ruto kuwa mpango wake wa nyumba, hata kama nia yake ni nzuri, Wakenya hawataki kabisa.
Wafanyakazi hasa pamoja na waajiri wao ndio hukatwa pesa hizi. Jinsi anavyofahamu, Wakenya wanaoathiriwa na makato hayo ni takribani 3 milioni.
Hizo ni kura ambazo huenda Dkt Ruto akapoteza katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata iwapo ameungwa mkono na aliyekuwa waziri mkuu Bw Raila Odinga, nyingi ya hizo kura za wafanyakazi atazipoteza.
Baadhi ya wakosoaji wa Rais wanasema mbali na wafanyakazi hao, hata wake au waume wao huenda wakamnyima Rais kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Ikumbukwe kuwa ushuru huu ulipigwa marufuku na mahakama mnamo 2024 kutokana na ubaguzi. Mahakama ilisema dosari ya ushuru huo ni kuwa ulilenga walioajiriwa pekee.
Baadaye serikali ilirejesha Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu bungeni na kuufanyia marekebisho.
Marekebisho hayo yalilenga kuwajumuisha Wakenya wengine katika ushuru huo wakiwemo bodaboda, mama mboga, wenye biashara na kadhalika.
Ni kwa msingi huo ambapo mahakama ilikubali na kuuruhusu ushuru huo uendelee. Lakini kinachosikitisha ni kuwa bado ni wafanyakazi pekee wanaokatwa kodi hiyo.
Kwa hivyo, ni muhimu Serikali mpya Jumuishi inapoundwa, Kenya Kwanza ianze kubadili baadhi ya sera zake maadamu hazipendwi na raia wengi.
Wataalamu mbalimbali wamependekeza kuwa njia rahisi ya kuimarisha SHA ingekuwa kuboresha bima ya kitaifa ya zamani (NHIF) wala si kuanzisha mfumo mpya kabisa.
Aidha, mfumo uliokuwepo wa ufadhili wa wanafunzi wa vyuo ungeimarishwa tu kwa kuongeza kiwango cha mkopo kutoka kwa Halmashauri ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB), na mgao wa serikali wa kila mwaka.
Lakini serikali ya Dkt Ruto ilionekana kulenga kujipiga kifua kwa kufutilia mbali kila jambo lililokuwepo na kuanza jipya kabisa.
Hapo kasoro ikatokea ndiyo maana kila kitu kimekwama.
Hata hivyo, serikali ina fursa nyingine nadra.
Ishauriwe na viongozi wa ODM waliojiunga nayo katika Serikali Jumuishi.