Wakulima wagutuka kusikia Mumias haijalipa ushuru wa Sh3.5 bilioni

0

WAKULIMA wa miwa Mumias wanataka Meneja Mrasimu wa Kiwanda cha Sukari cha Mumias Ponangipalli Venkata Ramana Rao achunguzwe kutokana na deni la Sh3.5 bilioni la ushuru.

Hii ni baada ya Jopo la Kuchunguza Ulipaji wa Ushuru kuipa idhini Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ruhusa ya kutwaa mali ya Mumias kulipa deni hilo.

Aliyekuwa Mbunge wa Mumias Wycliffe Osundwa ni kati ya viongozi ambao waliuliza jinsi ambavyo Bw Rao amekuwa akisimamia kiwanda hicho na kukosa kulipa ushuru.

“Bw Rao alipojiunga na Mumias Sugar alipata maguni 700 ya sukari, kila gunia likiwa na uzito wa kilo 50 na yenye thamani ya Sh4.2 milioni. Pia, kulikuwa na lita 685,000 za ethanol zenye thamani ya Sh274 milioni na miwa iliyokuwa tayari kuvunwa yenye thamani ya Sh170 milioni. Je, pesa hizi zilienda wapi?” akauliza Bw Osundwa.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Mumias, Bw Osundwa alisema kuwa kampuni  nyingine ambazo pia zilikuwa zimenunua ethanoli kwa mkopo zililipa.

Rais William Ruto akivuna miwa katika shamba moja Mumias Jumatatu. Picha|PCS

“Meneja anayesimamia kampuni hii kwa njia ya urasimu alianza uzalishaji wa ethanoli Februari 2020 hadi Desemba 2021. Alizalisha jumla ya lita milioni 2.2, zenye thamani ya Sh880 milioni. Inashtua kwamba faida ilipatikana lakini Bw Rao hakulipa ushuru,” alidai Bw Osundwa.

Wakulima hao na viongozi wa eneo hilo wanataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchunguza utata fedha hizo, katika kipindi cha Septemba 20, 2019 hadi Desemba 21, 2021.

Mkulima wa miwa kutoka Matungu, Bw Raphael Welimo, alidai kuwa kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, uharibifu mkubwa umekuwa ukifanyika kwenye mitambo ya ethanoli na umeme wa joto (co-gen) ndani ya kiwanda cha Mumias Sugar.

“Mnamo Februari 25, 2025, mshukiwa mmoja alikamatwa na akaandikisha taarifa OB No 09/25/2/2025. Tunafahamu kuwa mtambo wa ethanoli uliharibiwa na hata mshukiwa alikamatwa, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa licha ya uongozi kufahamu.”

Wakulima hao wametoa makataa ya siku 14 kwa Bw Rao kutangaza hali halisi ya kampuni hiyo, la sivyo wataanzisha mchakato wa kisheria kuipinga KCB.

Kiwanda hicho, kiliwekwa chini ya usimamizi wa benki ya Kenya Commercial Bank (KCB) mnamo Septemba 20, 2019, kwa kushindwa kutimiza majukumu yake kutokana na madeni mengi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *