Wezi watatu wauawa Jomvu kwa kumbaka na kumuibia msichana aliyekuwa ‘anatafuta mapenzi’

0

WEZI watatu wa kimabavu waliuawa na umati wenye ghadhabu katika eneo la Jitoni, Jomvu, mapema Alhamisi asubuhi, baada ya kumbaka na kumuibia msichana mmoja kwa kutumia njia ya udanganyifu mtandaoni.

Kwa miezi kadhaa, genge hili limekuwa likiwahangaisha wakazi wa Mombasa kwa visa vya wizi, unyanyasaji na dhuluma.

Kulingana na polisi, watuhumiwa hawa walimdanganya mwanamke huyo kupitia programu ya kuchumbiana mtandaoni kabla ya kumteka nyara, kumbaka na kumuibia.

Lakini hawakujua kuwa gari walilotumia—aina ya Honda Fit—lilikuwa likifuatiliwa kwa GPS na mmiliki wake.

Tukio hili lilianza Jumatano alasiri, wakati mshukiwa mmoja, Ali Mustafa, alikodisha gari hilo kutoka kwa kampuni ya Robmatt Car Hire Services huko Changamwe.

Alipaswa kulirudisha ifikapo saa tatu usiku, lakini muda ulipozidi kuyoyoma bila dalili ya kurejesha gari, mmiliki wake, Robert Kisavi, alianza kuwa na wasiwasi.

Wakati huo huo, genge hili lilikuwa likitekeleza njama yao. Kwa kutumia akaunti bandia ya kuchumbiana, walimshawishi mwanamke mmoja kutoka Bamburi akutane na “mchumba” wake mtarajiwa.

Lakini alipoketi ndani ya gari, hali ilibadilika. Alitishiwa kwa kisu na kisha akapitia mateso kwa saa kadhaa.

Waliendesha gari kutoka Bamburi, kupitia Nyali hadi katikati ya jiji la Mombasa, wakimdhulumu na kumuibia Sh4,200.

Bw Kisavi, aliyekuwa akifuatilia gari lake kwa GPS, aliona likielekea upande tofauti kupitia daraja la Nyali.

“Nilidhani labda mshukiwa alikuwa njiani kurudisha gari, lakini hilo halikutokea,” alisema.

Alipoona mwelekeo wa gari haukuwa wa kawaida, aliamua kuchukua hatua. Akiwa na rafiki yake na mteja mwingine aliyekuwa akisubiri kukodisha gari hilo, walianza msako.

Jitihada zao ziliwaleta hadi kituo cha mafuta Jomvu, ambapo waliona gari lililopotea likiwa limeegeshwa.

Lakini kabla hawajajua la kufanya, watuhumiwa walimtambua Bw Kisavi na kutimua mbio. Waliendesha kwa kasi kuelekea Jitoni wakijaribu kukwepa mkono wa sheria.

Walipoona wamezidiwa, waliliacha gari na kujaribu kukimbia kwa miguu huku wakimvuta mwathiriwa wao.

Ilipofika saa tisa usiku, mwanamke huyo aliona nafasi yake ya mwisho ya kuokoka.

Kwa sauti ya juu alipiga mayowe, akichana kimya cha usiku. Ni mwezi wa Ramadhani, na watu wengi walikuwa bado macho.

Sauti yake kali iliwavuta wakazi nje ya nyumba zao.

“Tunashukuru lilikuwa Ramadhani. Wananchi waliposikia kilio chake, waliamka haraka na kuwazingira wahalifu hawa,” shahidi mmoja alisimulia.

Hasira za wanakijiji zilizokuwa zimejengwa kwa muda kutokana na ongezeko la uhalifu zililipuka.

Umati uliwacharaza wahalifu hao kwa mawe, magongo na silaha nyinginezo hadi wakapoteza maisha.

Polisi walipofika, walikusanya vielelezo muhimu kutoka eneo la tukio, vikiwemo koti la polisi, bereti na kondomu zilizotumika.

Kamanda wa Polisi wa Mombasa, Peter Kimani, alieleza kuwa genge hilo limekuwa likisakwa kwa muda mrefu.

“Hii ni habari njema kwa wakazi wa Mombasa waliokuwa wakiishi kwa hofu,” alisema.

Pia alimsifu Bw Kisavi kwa hatua aliyochukua, akisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kupambana na uhalifu.

“Tunawahimiza wamiliki wa magari kufunga vifaa vya kufuatilia GPS na wafanyabiashara kutumia CCTV,” aliongeza.

Aidha, aliwataka wananchi kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kuchumbiana.

“Uhalifu umehamia mtandaoni. Watu wanapaswa kuwa makini wanapokutana na wageni,” alionya.

Kwa sasa, mwathiriwa anapokea matibabu na ushauri wa kisaikolojia huku polisi wakiendelea kuchunguza simu za watuhumiwa ili kubaini iwapo walikuwa na washirika wengine.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *